" SERIKALI YAWEKEZA BILIONI 218 KATIKA ELIMU, AFYA NA BARABARA MBEYA – PROF. SHEMDOE

SERIKALI YAWEKEZA BILIONI 218 KATIKA ELIMU, AFYA NA BARABARA MBEYA – PROF. SHEMDOE

Na: OWM–TAMISEMI, Mbeya

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amesema Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliridhia kutolewa kwa shilingi bilioni 75 mkoani Mbeya ambapo sehemu ya fedha hizo zilitumika kujenga shule mpya 57, madarasa 1,100 na nyumba za walimu 23. 

Aidha, amesema katika mwaka wa fedha 2026/27, Serikali imetenga shilingi bilioni 5.2 ambapo sehemu ya fedha hizo zitatumika kujenga madarasa 1,100 ili kujiandaa kuwapokea wanafunzi watakaoanza kidato cha kwanza mwaka 2028 kupitia mfumo wa double cohort.

Prof. Shemdoe ameyasema hayo Oktoba 16, 2026, baada ya kupewa fursa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, kueleza hatua zinazochukuliwa na OWM–TAMISEMI kutatua kero na changamoto za wananchi wa Jiji la Mbeya, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mwanjelwa, wakati wa ziara ya Makamu wa Rais ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani Mbeya.

“Mwaka huu tuna shilingi bilioni 5.2 ambazo zitatumika kujenga madarasa 1,100 ili kujiandaa kupokea wanafunzi wanaomaliza darasa la saba na darasa la sita, watakaoanza kidato cha kwanza mwaka 2028 kwa mfumo wa double cohort, ikiwa ni matokeo ya utekelezaji wa mtaala mpya,” amesema Prof. Shemdoe.

Katika sekta ya afya, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza shilingi bilioni 47 mkoani Mbeya kati ya mwaka 2021 na 2026, ambapo sehemu ya fedha hizo zimetumika kujenga zahanati 287, vituo vya afya 33 na hospitali tatu za halmashauri. 

Kwa upande wa barabara, Prof. Shemdoe amesema Serikali imewekeza shilingi bilioni 96 katika Jiji la Mbeya kati ya mwaka 2021 na 2026, ambapo sehemu ya fedha hizo zilizotumika kujenga barabara zenye urefu wa kilomita 96, zikiwemo kilomita 12.3 zilizojengwa kupitia mradi wa TACTIC, na kwa mwaka huu wa fedha imetenga shilingi bilioni 22.5 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za mijini na vijijini.

Uwekezaji huo wa shilingi bilioni 218 mkoani Mbeya katika elimu, afya na barabara, uliofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni hatua muhimu katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kuimarisha huduma za kijamii, kuchochea shughuli za kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

Post a Comment

Previous Post Next Post