" TAKWIMU ZA SARATANI ZATAJWA MSINGI WA KUBORESHA HUDUMA ZA MATIBABU

TAKWIMU ZA SARATANI ZATAJWA MSINGI WA KUBORESHA HUDUMA ZA MATIBABU

 


Na, Egidia Vedasto, APC Media, Arusha

KCRI Yataka Takwimu Sahihi Katika Udhibiti wa Saratani

Profesa Blandina Mmbaga, Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (KCRI), kilichopo chini ya Hospitali ya Rufaa ya KCMC, amesema kongamano hilo limewakutanisha wataalamu na wabobezi wa masuala ya saratani, hususan saratani ya shingo ya kizazi, matiti na aina mbalimbali za saratani.

Akizungumza katika Mkutano wa Kwanza wa Pamoja wa Kisayansi wa Mitandao Mitatu ya Kimataifa ya Ufuatiliaji na Utafiti wa Saratani Jijini Arusha, amesema lengo kubwa la kongamano hilo ni kujadili namna bora ya kutunza na kutumia takwimu za saratani katika nchi mbalimbali, ili kusaidia katika kupanga mikakati ya kinga, uchunguzi na matibabu ya ugonjwa huo.

Aidha amesema jumla ya nchi 25 kutoka bara la Ulaya zimeshiriki katika kongamano hilo, sambamba na takribani nchi 35 kutoka bara la Afrika, ambapo wataalamu hao wamekutana kujadili changamoto zinazowakabili katika udhibiti wa saratani.

Profesa Mmbaga amesema "kupitia kongamano hili wataalamu wanaangalia umuhimu wa kuwa na takwimu za wagonjwa Ili kubaini ukubwa wa tatizo la saratani, ikiwemo kubaini aina za saratani zinazoongoza, maeneo ambayo ugonjwa huo umeenea zaidi pamoja na makundi ya umri yanayoathirika, ili wagonjwa wanaogundulika waweze kupata matibabu mapema".


Amesema pia wanafunzi wa masuala ya saratani wamejengewa uwezo wa kutambua dalili za saratani, ikiwemo kubaini vimbe zinazoweza kuwa na dalili za ugonjwa huo, pamoja na kupata uelewa kuhusu namna ya kuwahudumia na kuwatibu wagonjwa.

Vilevile ameeleza kuwa katika kufanikisha azma hiyo, wataalamu kutoka KCRI wamekuwa wakishirikiana pia na waganga wa jadi, kwa kuwa baadhi ya wagonjwa baada ya kugundulika wamekuwa wakikimbilia kwao. Amesema masheikh na wachungaji nao wanahusishwa katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa uchunguzi wa saratani na kuwahamasisha wagonjwa kupata huduma za matibabu kwa wakati.

Kwa upande wake Prof. Gileard Masenga Mkurugenzi wa hospitali ya Rufaa ya Kanda ya kaskazini KCMC  amesema magonjwa yasiyoambukiza yanaendelea kuongoza miongoni mwa wagonjwa wanaofika hospitalini kupata huduma za afya, ambapo kati ya wagonjwa 10, takribani wanane hugundulika kuwa na magonjwa hayo, ikiwemo saratani, shinikizo la damu, kisukari na madhara yatokanayo na ajali.


Amesisitiza umuhimu wa kuwa na takwimu sahihi za afya ili kubaini ukubwa wa tatizo la saratani na magonjwa mengine, hali itakayosaidia wataalamu na Serikali kupanga mikakati madhubuti ya kinga, uchunguzi na matibabu.

Prof. Masenga, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya afya, hususan katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, akieleza kuwa Juni 20 mwaka huu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua huduma ya tiba ya mionzi kwa wagonjwa wa saratani. Amesema kwa sasa KCMC wanaendelea kutoa matibabu ya saratani kwa kutumia mionzi.


Katika namna hiyo hiyo Mkurugenzi wa Huduma za afya, uzazi mama na mtoto kutoka Wizara ya Afya Dkt. Ahmed Mohamed Makuwani amesisitiza umuhimu wa taasisi za afya kuwa na vitabu vya takwimu kwa lengo la kuwa na kumbukumbu halisi za utoaji wa huduma za afya, ambazo zitasaidia katika kupanga mipango mizuri ya kukabiliana na magonjwa mbalimbali.

Amesema takwimu hizo zitasaidia kujua visababishi vya magonjwa, idadi ya wagonjwa pamoja na maeneo yanayoongoza kwa kuwa na wagonjwa wa saratani na makundi ya umri yanayoathirika zaidi.

Ameeleza kuwa taarifa hizo zitasaidia kuboresha huduma za afya na kupanga mahitaji ya watumishi katika hospitali zinazotoa huduma za matibabu ya saratani, ikiwemo Hospitali ya Ocean Road, KCMC na Bugando.

Post a Comment

Previous Post Next Post