Na, Egidia Vedasto, Misalaba Media, Arusha.
Mkuu wa mkoa wa Arusha CPA Amos Makalla baada ya kuwaapisha wakuu wa Wilaya wapya wa Wilaya za Arumeru, Ngorongoro na Arusha, amebainisha kuwa hana mashaka na viongozi hao na kuwatakia kila la heri katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akizungumza mara baada ya kuwaapisha viongozi hao, amewaahidi ushirikiano wa karibu katika kusukuma maendeleo wananchi.
Aidha amesema kuwa Arusha ni mkoa wa pili kwa ukusanyaji wa mapato nchini baada ya Dar es Salaam, huku ukiwa kitovu cha utalii, diplomasia na utalii wa mikutano, michezo pamoja na utalii wa kitabibu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa ccm mkoa wa Arusha Thomas ole Sabaya amewataka Wakuu hao wa Wilaya kuhakikisha usafi na utunzaji wa mazingira vinafanyika muda wote katika maeneo yao, huku wakitekeleza kauli ya Rais ya kuhakikisha wananchi wanaishi kwa furaha na kuachwa na tabasamu.
Pia amewapongeza wakuu wa Wilaya waliostaafu kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kusukuma maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.Sambamba na hayo, amewapongeza wakuu wa Wilaya walioapishwa na kuwatakia kila la heri katika utekelezaji wa majukumu yao, huku akiwaomba kutekeleza ahadi za Rais, kusikiliza wananchi na kuhakikisha wanatatua na kumaliza kero zinazowakabili katika maeneo yao.
Vile vile Waziri wa habari, sanaa, utamaduni na michezo na Mbunge wa Arusha Paul Makonda amesisitiza viongozi kufanya kazi kwa bidii, kushirikiana, kuhimiza usafi na kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa wananchi.
Amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira yatakayowezesha wananchi kunufaika na fursa mbalimbali za maendeleo na ameahidi kujenga msikiti wa kiutalii ambao utakuwa kivutio kwa wageni na wananchi, akieleza kuwa lengo ni kuhakikisha eneo hilo linakuwa kivutio kikubwa cha utalii ndani ya miaka mitano ijayo.
Mkuu wa wilaya mteule wa Wilaya ya Arusha Nicodemus Mwikozi amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua kuwa Mkuu wa Wilaya, akiahidi kufanya kazi kwa bidii, kuwatumikia wananchi na kuhakikisha anaendana na kasi ya maendeleo ya Mkoa wa Arusha.
Aidha, amewataka vijana wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu, wakiwemo vibaka, kuacha mara moja, akisema muda wao umeisha. Ameahidi kuweka taa za mitaani, kuhimiza usafi hususan katika maeneo ya vituo vya bodaboda na kuanza ziara katika mitaa yote ya wilaya mara baada ya kuapishwa rasmi.
PROFESSOR MGOKO EP 04
Post a Comment