" CHUNYA YAWEKA MSUKUMO MPYA KATIKA KUBORESHA MASLAHI YA WENYE ULEMAVU

CHUNYA YAWEKA MSUKUMO MPYA KATIKA KUBORESHA MASLAHI YA WENYE ULEMAVU


Na Lydia Lugakila- Misalaba MediaCHUNYA/MBEYA Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Dkt. Theodory Lukasi, amewataka wajumbe wa Kamati ya Watu Wenye Ulemavu wilayani humo kuwa mabalozi kwa wenzao katika jamii kwa kusambaza taarifa kuhusu elimu, fursa na masuala mbalimbali yanayohusu haki na maendeleo ya watu wenye ulemavu.Dkt. Lukasi ametoa wito huo novemba 6, 2026, wakati wa kikao cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha, Julai hadi Septemba, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwanginde, kwa ajili ya kuwasilisha na kujadili taarifa za utekelezaji wa shughuli mbalimbali zinazowahusu watu wenye ulemavu.Amesema wajumbe wa kamati hiyo wana nafasi muhimu ya kuhakikisha taarifa na maamuzi yanayojadiliwa katika vikao vinawafikia watu wenye ulemavu waliopo katika vijiji na kata mbalimbali ili nao waweze kunufaika na fursa zinazotolewa na Halmashauri.“Ninyi wajumbe wa Kamati ya Watu Wenye Ulemavu Wilaya ndio mabalozi wa kuyafikisha mambo mbalimbali yanayojadiliwa katika vikao kwa wenzetu walioko katika vijiji na kata zetu, ili nao waweze kunufaika na kile tunachokipata kupitia vikao hivi,” amesema Dkt. Lukasi.Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Bi. Lutness Mbise, amesema ofisi hiyo ina wajibu wa kuhakikisha watu wenye ulemavu wananufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri kwa makundi maalumu.Aidha amesisitiza umuhimu wa wanufaika kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kuwawezesha watu wengine wenye ulemavu kupata fursa hiyo, kama ilivyo kwa makundi mengine ya wanawake na vijana.Amesema urejeshaji wa mikopo ni sehemu muhimu ya kuhakikisha fedha hizo zinaendelea kuzunguka na kuwafikia wanufaika wengine wenye mahitaji.Naye Afisa Elimu Maalum wa Wilaya ya Chunya, Bi. Hawa Mtonyole, amewataka wajumbe wa kamati hiyo kuwa mabalozi wa kuhamasisha jamii kuhusu uwepo wa bweni katika Shule ya Msingi Kibaoni kwa ajili ya watoto wa kike wenye mahitaji maalum, ili wazazi na walezi wenye watoto hao waweze kuwapeleka shuleni kupata elimu katika mazingira rafiki.Aidha, amesema zoezi la kubaini watoto wenye mahitaji maalum wanaotarajia kuanza elimu ya awali na darasa la kwanza kwa mwaka wa masomo 2027 linaendelea, huku akiwataka wajumbe kutumia nafasi zao kuifikishia jamii taarifa hizo ili watoto wote wanaostahili waweze kutambuliwa na kuandikishwa shuleni.“Kwa sasa tunaendelea na zoezi la kubaini watoto wenye mahitaji maalum wanaotarajiwa kuanza darasa la awali na darasa la kwanza. Niwaombe wajumbe wote kuwa mabalozi katika maeneo yao kwa kuwafahamisha wazazi wenye watoto wenye umri wa miaka mitano kwa darasa la awali na miaka sita kwa darasa la kwanza kwa mwaka wa masomo 2027,” amesema Bi. Mtonyole.Katika kikao hicho, taarifa za utekelezaji wa shughuli mbalimbali kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha, Julai hadi Septemba, ziliwasilishwa na idara mbalimbali za Halmashauri, zikiwemo Idara ya Afya kupitia Kitengo cha Ustawi wa Jamii, Idara ya Elimu ya Msingi na Idara ya Maendeleo ya Jamii.Hata hivyo suala la urejeshaji wa mikopo ya asilimia 10 lilijadiliwa, huku watu wenye ulemavu wakihimizwa kutimiza wajibu wao wa kurejesha mikopo waliyopewa ili kuhakikisha fedha hizo zinaendelea kunufaisha makundi mengine yanayostahili.Kikao cha Kamati ya Watu Wenye ulemavu Wilaya ya Chunya hushirikisha wawakilishi wa makundi mbalimbali ya watu wenye ulemavu pamoja na wajumbe kutoka idara za Afya, Elimu ya Msingi, Elimu ya Sekondari na Maendeleo ya Jamii kwa lengo la kujadili, kufuatilia na kuweka mikakati ya kuboresha huduma na ustawi wa watu wenye ulemavu.Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Bi. Lutness Mbise, akizungumza.

PROFESSOR MGOKO EPISODE 07

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post