" TANESCO KUIMARISHA ZUZU KUPISHA MRADI WA TAZA

Top News

TANESCO KUIMARISHA ZUZU KUPISHA MRADI WA TAZA

📍Huduma ya Umeme kukosekana kwa saa maalumu Novemba 14 na 15 katika baadhi ya mikoa

Na.Alex Sonna DODOMA

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) linatarajia kufanya maboresho ya miundombinu ya kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Zuzu, mkoani Dodoma, Novemba 14 na 15, mwaka huu, ili kukiwezesha kufanya kazi kwa msongo wa kilovolti 400 (kV 400), ikiwa ni maandalizi ya kuwasha Mradi wa Usafirishaji Umeme wa Tanzania na Zambia (TAZA).

Utekelezaji wa kazi hizo utasababisha kusitishwa kwa huduma ya umeme katika baadhi ya maeneo ya Kanda ya Kaskazini, Magharibi na Ziwa, kuanzia saa 12:30 asubuhi hadi saa 11:30 jioni katika kila moja ya siku hizo mbili.

Maboresho hayo yanalenga kuongeza uwezo wa kusafirisha umeme, kuimarisha uhakika wa huduma nchini na kuwezesha muunganiko wa gridi za umeme za Tanzania na Zambia.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Novemba 12, 2026, jijini Dodoma, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO anayeshughulikia Usambazaji, Mhandisi Timothy Mgaya, amesema kazi hizo zitahusisha kuzima baadhi ya miundombinu ili kuiboresha na kuiwezesha kufanya kazi kwa msongo uliosanifiwa wa kV 400.

Amesema kwa sasa baadhi ya miundombinu ya kituo hicho inafanya kazi kwa msongo wa kV 220 kutokana na kutokamilika kwa maboresho ya kituo cha Iringa, hali iliyolazimu kuendelea kutumia kiwango hicho wakati utekelezaji wa mradi ukiendelea.

“Kwa sasa TANESCO inapokea umeme wa kV 400 kutoka kituo cha Julius Nyerere na kuufikisha Dodoma, ambako kituo cha Zuzu kinatarajiwa kuwa kitovu muhimu cha kusafirisha umeme huo kuelekea Iringa, Singida, Shinyanga na Arusha,” amesema Mhandisi Mgaya.

Ametaja mikoa itakayoguswa na kusitishwa kwa huduma hiyo kuwa ni Singida, Manyara, Arusha, Kigoma, Kagera, Tabora, Shinyanga, Simiyu, Geita, Mwanza na Mara.

Mhandisi Mgaya amesema TANESCO imejipanga kushirikiana na mkandarasi kuhakikisha kazi zinafanyika kwa usalama na ufanisi, na kukamilika ndani ya muda uliopangwa ili kupunguza usumbufu kwa wananchi na shughuli za kiuchumi.

Aidha, amesema shirika hilo litatumia njia mbalimbali kuwafahamisha wananchi kuhusu zoezi hilo, zikiwemo ujumbe mfupi wa simu, makundi ya WhatsApp, mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.

Amewaomba wananchi kuvumilia usumbufu huo wa muda wakati kazi zikiendelea, akieleza kuwa maboresho hayo ni muhimu katika kuimarisha huduma ya umeme.

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa Usafirishaji Umeme wa Tanzania na Zambia, Mhandisi Deogratius Nyamtumbaga, amesema kazi zitakazofanyika Novemba 14 na 15 zitawezesha kuboresha miundombinu ya kusafirisha umeme kutoka Dodoma kuelekea Iringa kwa msongo wa kV 400, ikiwa ni maandalizi ya kuwasha Mradi wa TAZA.

Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuwezesha usafirishaji wa umeme kutoka Iringa hadi Sumbawanga na hatimaye kuunganisha gridi ya Tanzania na Zambia.

“Maboresho hayo yatasaidia pia kuwasha njia ya pili ya kusafirisha umeme kutoka Dodoma kwenda Singida kwa msongo wa kV 400, hatua itakayoongeza uwezo wa miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini,” amesema Mhandisi Nyamtumbaga.

Ameeleza kuwa kituo cha Singida kitaongezewa transfoma nyingine yenye uwezo wa MVA 250, itakayofanya kazi pamoja na iliyopo ili kuongeza uwezo wa kituo hicho na kuimarisha upatikanaji wa umeme katika Kanda ya Kaskazini, Ziwa na Magharibi.

Akizungumzia maendeleo ya Mradi wa TAZA, amesema utekelezaji wake ulianza Novemba 2023 kwa ujenzi wa nguzo na njia za kusafirisha umeme, huku ujenzi wa vituo vya kupoza umeme ukianza Aprili 2024.

Amesema ujenzi wa njia za kusafirisha umeme umefikia asilimia 96, huku ujenzi wa vituo vya kupoza umeme ukiwa umefikia asilimia 94.

Mradi huo, wenye gharama ya takriban Sh trilioni mbili, unahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme yenye urefu wa kilomita 620 kutoka Iringa hadi Sumbawanga, pamoja na vituo vya kupoza umeme vya Iringa, Kisada, Mbeya, Tunduma na Sumbawanga.

Mhandisi Nyamtumbaga amesema TANESCO inatarajia kuanza kuwasha miundombinu ya kV 400 kutoka Dodoma hadi Iringa na Kisada mwishoni mwa Novemba, huku sehemu ya Mbeya hadi Sumbawanga ikitarajiwa kuwashwa Novemba 29, mwaka huu.

Ameeleza kuwa ifikapo Desemba 5, mwaka huu, wakazi wa Sumbawanga wanatarajiwa kuanza kupata umeme kutoka katika gridi ya taifa ya Tanzania badala ya kutegemea umeme kutoka Zambia kama ilivyo sasa.

Ameongeza kuwa kazi zilizosalia zinahusisha pia majaribio na uthibitishaji wa mifumo ili kuhakikisha miundombinu inafanya kazi kwa usahihi na usalama kabla ya mradi kuanza kutumika kikamilifu.

      

Post a Comment

Previous Post Next Post