Na Mapuli Kitina Misalaba
Waziri Mkuu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ametoa
maelekezo kwa viongozi na watendaji wa Serikali Nchini kuhakikisha changamoto
zinazowakabili wananchi katika sekta mbalimbali zinashughulikiwa, akisisitiza
kuwa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kutatua kero za
wananchi na kuboresha huduma za kijamii na kiuchumi.
Dkt. Mwigulu
ametoa maelekezo hayo leo Novemba 8, 2026, wakati akizungumza na maelfu ya
wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Wilaya ya Kishapu mkoani
Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi ya siku nne mkoani humo.
Katika
mkutano huo, Waziri Mkuu ametangaza kuwa kuanzia msimu ujao wa ununuzi wa
pamba, Serikali itaondoa mfumo wa kuwa na mnunuzi mmoja, akieleza kuwa hatua
hiyo inalenga kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika ununuzi wa zao
hilo na kuboresha mazingira ya wakulima.
Akizungumzia
sekta ya afya, Dkt. Mwigulu ameeleza kutoridhishwa na taarifa za baadhi ya
vituo vya afya, zahanati na hospitali Nchini kuripoti kupokea dawa kutoka
Serikalini, lakini wagonjwa wanapofika kuhitaji dawa hizo huambiwa hazipo na
kuelekezwa kuzinunua katika maduka ya dawa.
Amehoji
chanzo cha upatikanaji wa dawa hizo katika maduka ya nje ya vituo vya kutolea
huduma za afya wakati wagonjwa wakielezwa kuwa hazipatikani katika vituo vya
Serikali, huku akivielekeza vyombo vya dola kufuatilia taarifa hizo ili kubaini
ukweli na kuchukua hatua stahiki.
Aidha,
amepiga marufuku utaratibu wa kuwachelewesha wagonjwa mahututi na wajawazito
wanaofika hospitalini wakiwa katika hali inayohitaji huduma ya haraka kwa
sababu ya taratibu za usajili, akielekeza wagonjwa hao wapatiwe matibabu kwanza
na taratibu za kiutawala zifuatwe baadaye.
Katika hatua
nyingine, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma, wakiwemo madaktari, kuacha
kutumia muda wa kazi kuchati na kufanya shughuli zisizohusiana na majukumu yao,
akisisitiza umuhimu wa kuwahudumia wananchi wanaofika katika ofisi za Serikali
kutafuta huduma.
Amesema si
sahihi kwa mtumishi wa umma kukataa kumsikiliza mwananchi anayefika ofisini kwa
kisingizio kwamba hana miadi maalumu (appointment), ilhali mwananchi huyo
ametumia muda na gharama kufika kupata huduma.
“Nimepata
nafasi ya kufanya kazi na Rais Samia, ameshatimiza wajibu wake. Sisi wengine
Watanzania, hasa tunaomsaidia huku chini, tunatakiwa tutimize wajibu wetu,”
amesema Dkt. Mwigulu.
Kuhusu
changamoto zinazowakabili waendesha vyombo vya usafiri wa kibiashara wakiwemo
bodaboda na bajaji nchini, Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua umuhimu wa
vyombo hivyo katika kuwaingizia kipato wananchi, hivyo ameelekeza kuwepo kwa
utaratibu utakaowawezesha wanaokosea kulipa faini bila kunyang'anywa vyombo
vyao vya usafiri.
Ameeleza
kuwa baadhi ya waendesha bodaboda na bajaji wanatumia vyombo vilivyonunuliwa
kwa mikopo, hivyo kuvichukua na kuvihifadhi hadi wahusika watakapolipa faini
kunawaongezea ugumu wa kupata kipato cha kulipa adhabu hizo.
Katika sekta
ya ujenzi, Dkt. Mwigulu amesema Serikali imefuta kodi za uingizaji saruji
kutoka nje ya nchi pamoja na malighafi zinazotumika katika uzalishaji wa
saruji, hatua ambayo amesema inalenga kupunguza gharama za uzalishaji na
kuifanya bidhaa hiyo kupatikana kwa bei nafuu zaidi.
Amesema
hatua hiyo inatarajiwa kuchangia kushuka kwa bei ya saruji katika siku zijazo,
jambo litakalosaidia wananchi wanaojenga na kuendeleza shughuli mbalimbali za
ujenzi.
Aidha,
ameelekeza changamoto za miundombinu ya barabara na upatikanaji wa maji katika
Wilaya ya Kishapu na Mkoa wa Shinyanga kwa ujumla kushughulikiwa ili kuboresha
huduma na kuchochea shughuli za kiuchumi kwa wananchi.
Kwa upande
wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amemshukuru Waziri Mkuu kwa
kutembelea mkoa huo na kupata fursa ya kuzungumza moja kwa moja na wananchi,
akieleza kuwa ziara hiyo ni muhimu katika kuimarisha mawasiliano kati ya
Serikali na wananchi.
Katika taarifa
yake Mhe. Mhita amesema Mkoa wa Shinyanga unaendelea kusimamia utekelezaji wa
miradi ya maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma za kijamii, huku akibainisha
kuwa ushirikiano kati ya Serikali Kuu, viongozi wa mkoa, wilaya na Halmashauri
ni muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo.
Ameeleza
kuwa maelekezo yaliyotolewa na Waziri Mkuu yatakuwa mwongozo kwa viongozi na
watendaji katika maeneo yao ya kazi, hususan katika kushughulikia kero za
wananchi na kuhakikisha changamoto zinazowasilishwa zinapatiwa ufumbuzi.
Mkutano huo
umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, akiwemo Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi Patrobas Katambi, Waziri wa Ujenzi Masanja Kungu Kadogosa, Naibu
Waziri wa Nishati Salome Makamba, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –
TAMISEMI Dkt. Jafar Seif na Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Kundo Andrea Mathew.
Wengine
waliohudhuria ni Mbunge wa Jimbo la Kishapu Mhe. Lucy Mayenga, Mkuu wa Wilaya
ya Kishapu Peter Nicholaus Masindi, Mkuu wa Wilaya ya Kahama Dkt. Francis Daud
Mlacha, pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro.
Maelfu ya
wananchi, wakiwemo viongozi wa dini, viongozi wa kimila na wawakilishi wa
taasisi za umma na binafsi kutoka ngazi za mkoa, wilaya na kata, wamehudhuria
mkutano huo.
Katika
mkutano huo, Waziri Mkuu pia amepata fursa ya kusikiliza kero na changamoto
zilizowasilishwa na wananchi na kutoa maelekezo ya kuzishughulikia mbele ya
wananchi hao.
Ziara ya
Waziri Mkuu inaendelea kesho Novemba 9, 2026, ambapo atatembelea na kufanya
mikutano ya hadhara katika Jimbo la Solwa ambapo ni Halmashauri ya Wilaya ya
Shinyanga, pamoja na Jimbo la Shinyanga Mjini ndani ya katika Halmashauri ya
Manispaa ya Shinyanga.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, akizungumza na maelfu ya wananchi waliojitokeza katika mkutano wa hadhara Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga leo Novemba 8, 2026.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, akizungumza katika mkutano wa hadhara wa Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba uliofanyika Wilaya ya Kishapu, akieleza masuala mbalimbali ya maendeleo ya mkoa huo.
aziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.
Waziri wa Ujenzi, Masanja Kungu Kadogosa, akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa Waziri Mkuu uliofanyika Wilaya ya Kishapu.
Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi CCM Mkoa wa Shinyanga Mhe. Mabala Mlolwa akizungumza kwenye mkutano huo.
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba Wilaya ya Kishapu.
Viongozi wa Serikali, viongozi wa dini, viongozi wa kimila na wananchi mbalimbali wakiwa katika mkutano wa hadhara wa Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba Wilaya ya Kishapu.
Viongozi wa Serikali, viongozi wa dini, viongozi wa kimila na wananchi mbalimbali wakiwa katika mkutano wa hadhara wa Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba Wilaya ya Kishapu.
Viongozi wa Serikali, viongozi wa dini, viongozi wa kimila na wananchi mbalimbali wakiwa katika mkutano wa hadhara wa Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba Wilaya ya Kishapu.
Viongozi wa Serikali, viongozi wa dini, viongozi wa kimila na wananchi mbalimbali wakiwa katika mkutano wa hadhara wa Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba Wilaya ya Kishapu.
Viongozi wa Serikali, viongozi wa dini, viongozi wa kimila na wananchi mbalimbali wakiwa katika mkutano wa hadhara wa Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba Wilaya ya Kishapu.
Viongozi wa Serikali, viongozi wa dini, viongozi wa kimila na wananchi mbalimbali wakiwa katika mkutano wa hadhara wa Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba Wilaya ya Kishapu.
Viongozi wa Serikali, viongozi wa dini, viongozi wa kimila na wananchi mbalimbali wakiwa katika mkutano wa hadhara wa Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba Wilaya ya Kishapu.

Awali , Mkuu
wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita akimpokea Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.

PROFESSOR MGOKO EPISODE 07
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254






























Post a Comment