" MZEE NALINGA MWENYE UMRI WA MIAKA ZAIDI YA MIA MOJA (100) ATUMA UJUMBE KWA RAIS, SERIKALI NA JAMII KUHUSU MIAKA 61 YA UHURU.

MZEE NALINGA MWENYE UMRI WA MIAKA ZAIDI YA MIA MOJA (100) ATUMA UJUMBE KWA RAIS, SERIKALI NA JAMII KUHUSU MIAKA 61 YA UHURU.

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Mzee Nalinga Najulwa mwenye umri wa Miaka 103 anayeishi mtaa wa Dome kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga amesema Tanzania inapofikisha Miaka 61 ya uhuru suala la maadili liwe ajenda ili kuendelea kuwa na Taifa lenye kizazi chenye uadilifu.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na Misalaba Blog ambapo amesema licha ya mabadiliko mbalimbali yanayojitokeza suala la maadili limeendelea kusahaulika hali inayochangia kuwa na kizazi kinachorithi mmomonyoko wa maadili.

Mzee Najulwa ameiomba jamii kuheshimu maadili ya kitanzania badala ya kufuata tamaduni za mataifa ya Magharibi ambazo baadhi yake zinamafundisho yanayosababisha madhara ikiwemo vitendo vya ukatili katika jamii.

Amewataka viongozi wa dini kutumia nafasi yao kutoa mafundisho kwa waumini wao waweza kuwa na hofu ya Mungu ili kuondokana na vitendo viovu.

“Hii inasababishwa na baadhi ya watu kuwa na tamaa katika Dunia hii nawaomba sana viongozi wa Dini na kwenye misikiti wanatakiwa wafanye bidii sana kuwaelimisha watu ili wawe karibu na uchaji wa Mungu maana wameshayaacha mambo ambayo Mungu ameagiza wanajifanya wao wenyewe”.amesema Mzee Nalinga Najulwa

Mzee Najulwa ametumia nafasi hiyo kuiomba serikali kuwa na utamaduni wa kuielezea historia ya uhuru wa Tanganyika kwa njia mbalimbali ikiwemo mikutano ya hadhara ili kuwawezesha kuwa na kumbukumbu nzuri juu ya Nchi yao.

“Viongozi wa serikali wakazane kuwaelimisha watu na wawe na utaratibu wa kufanya mikutano ya kuwaelezea wapate elimu hiyo ya kumbukumbu kuwakumbusha mambo yalivyokuwa tangu Mwanzo lakini pia Rais anatakiwa awe karibu na watu kwa ajili ya kuwaelezea jinsi utawala unavyoendeleo”.amesema Mzee Nalinga

Aidha Mzee Nalinga Najulwa amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuungana na viongozi wengine marais wa awamu zilizopita kuendeleza umoja katika Taifa la Tanzania.

Leo Disemba 9, 2022 ni siku ya  Kumbukumbu ya Maadhimisho ya Miaka 61 ya uhuru wa Tanganyika ambayo huadhimishwa kila Mwaka ifikapo Mwezi na tarehe kama ya leo.

Post a Comment

Previous Post Next Post