Wakati vita dhidi ya ukeketaji vikiendelea, ripoti ya ziara ya siku 16 ya kupinga ukatili wa kijinsi imebaini kuwapo kwa biashara ya viungo vya siri vinavyotolewa kwa wasichana wanaokeketwa.
Viungo hivyo baada ya kutolewa huuzwa kwa wafanyabiashara wa madini na wavuvi kwa kati ya Sh1 milioni hadi Sh20 milioni kutegemea wingi wake.
Hayo yameelezwa katika maadhimisho ya siku za haki za binadamu yaliyoandaliwa na Mtandao wa watetezi wa haki za binadamu, huku wakiitaka Serikali kufanyia marekebisho sheria ya ndoa, kutunga mpya itakayokemea unyanyasaji wa kijinsia na kufanya mabadiliko ya sheria inayosimamia mashirika yasiyo ya kiserikali.
Akiwasilisha ripoti ya ziara ya siku 16 katika mikoa minane nchini, Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Makundi Maalumu, Josiah Saoke alisema biashara hiyo ya viungo imekuwa ikichochea ukeketaji.
“Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na wananchi wakati wa kampeni hii, wasichana wanapokeketwa viungo vyao huuzwa kwa wafanyabiashara wakubwa wa madini na wa samaki ambao wanaamini vinaongeza wingi wa madini na samaki,” alisema.
Alisema hilo linamaanisha kuwa tatizo la ukatili wa kijinsia ni zaidi ya mila na desturi kama ilivyozoeleka.
“Hivyo, upo umuhimu wa Serikali na wadau kufanya utafiti ili kugundua wanaonufaika na biashara hii ili wachukuliwe hatua za kisheria,” alisema.
Kutokana na vitendo vya ukeketaji kupigwa marufuku nchini, ripoti hiyo imebainisha kuwa hivi sasa wazazi waliodhamiria kufanya vitendo hivyo hulazimika kuvuka mipaka kwenda Kenya kukamilisha tohara hiyo.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) msichana mmoja kati ya 10 aliye na umri wa miaka 15 hadi 49 nchini Tanzania amekeketwa.
Kampeni hiyo ilihusisha msafara wa wanaharakati ambao ulizunguka mikoa ya Pwani, Morogoro, Singida, Shinyanga, Geita, Mara na Arusha, kwa ajili ya kupaza sauti kupinga ukatili wa kijinsia.
Kati ya changamoto iliyobainika ni baadhi ya watendaji wa Serikali, wakiwamo polisi na mahakimu kulalamikiwa kupokea rushwa kwa watuhumiwa wa vitendo vya ukatili wa kijinsia.
“Hii inapelekea kuharibiwa kwa ushahidi, kucheleweshwa kwa kesi hivyo kutopatikana kwa haki kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia,” alisema.
Akizungumzia suala hilo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima alisema atakwenda kushirikiana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi ili kufuatilia suala hilo.
“Hili ni jambo zito sana, nalichukua vilivyo asanteni kwa kuliibua, tunakwenda kulichunguza vizuri ili tuwapate hao watu wanavyofanya hivi vitu kwani sasa ni biashara kubwa sana, imetoka kwenye mila inaenda kwenye ushirikina. Niwatangazie waganga ambao hawajasajiliwa na wako kwenye jamii wanafanya utapeli na kuuza viungo vya watu sasa wamehamia kwenye viungo vya siri vinavyofanyiwa ukeketaji wanavichukua eti wanaenda kuvifanyia sijui shughuli gani huu ni ukatili mpya kabisa ambao umeanza,” alisema Waziri Dorothy.
Alisema kwa kushirikiana na Waziri wa mambo ya ndani watakwenda kushughulikia suala hilo ili kupata vidhibiti pale itakapohitajika.
Mkurugenzi wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendelo Afrika (Wildaf), Anna Kulaya alisema moja ya changamoto ya mapambano dhidi ya ukatili ni kukosekana kwa sheria ya kudhibiti ukatili wa kijinsia.
“Uwepo wa hii sheria utasaidia wahanga wengi kupata haki zao kwa wakati, pia sheria ya ndoa bado kuna tatizo na sheria ya mirathi nayo. Kama hakutakuwa na sheria inayowalinda wanawake, wasichana na watoto bado civic space inaenda kuwaathiri,” alisema Anna.
Post a Comment