Na Mapuli Kitina Misalaba
Mfanyakazi wa ndani aitwaye Neema Justine mwenye umri
wa Miaka 19, mkazi wa Kata ya Old Shinyanga, amefariki dunia kwa tuhuma za
kujinyonga ndani ya nyumba aliyokuwa akiishi, tukio lililotokea majira ya
mchana.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Soko B, Kijiji cha Old
Shinyanga, Bwana Leonardo Magige amesema alipokea taarifa za tukio hilo majira
ya saa sita mchana na kufika haraka eneo la tukio kwa ajili ya kufuatilia
kilichotokea.
Amesema kwa mujibu wa maelezo ya familia, siku ya
tukio mama mwenye nyumba alikuwa akifanya shughuli za kufua nguo asubuhi,
ambapo baadaye mfanyakazi huyo wa ndani naye alieleza kuwa ana nguo zake za
kufua. Hata hivyo, mama huyo aliamua kufua nguo hizo kabla ya kuondoka kwenda
kazini.
Kabla ya kuondoka, mama huyo aliondoka na mtoto wake
kwenda kazini kwake (dukani) ambapo alimpatia mtoto wake hela kwa ajili ya kununua
mahitaji ya chakula, na aliporudi nyumbani alimkuta Neema akiwa tayari
amefariki kwa kujinyonga dirishani bila kuacha ujumbe wowote.
“Baada ya kupata taarifa hizo,
niliwasiliana na polisi wa kata ambao nao walitoa taarifa kituo cha polisi.
Maafisa walifika eneo la tukio na kuchukua mwili wa marehemu kuupeleka katika
Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga kwa uchunguzi zaidi,”
amesema Magige.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi
Mwandamizi wa Polisi Janeth Magomi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na
kusema uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo chake.
“Tulipokea taarifa kutoka kwa Evaline Richard
aliyegundua kifo cha mfanyakazi wake wa ndani, Neema Justine, ambaye alifariki
kwa kujinyonga ndani ya nyumba aliyokuwa akiishi. Hadi sasa chanzo
hakijajulikana kwani hakukuwa na ujumbe wowote ulioachwa,” amesema Kamanda
Magomi.
SACP Magomi ametoa wito kwa wazazi, walezi na jamii
kwa ujumla kuimarisha malezi na mawasiliano ndani ya familia, pamoja na
kuwachukulia wafanyakazi wa ndani kama sehemu ya familia ili kuwapa mazingira
salama ya kuishi.
Naye Mwenyekiti wa Kitongoji, Magige, amesisitiza
umuhimu wa wazazi kuwa karibu na watoto wao ili waweze kueleza changamoto
wanazokutana nazo bila hofu.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya
Manispaa ya Shinyanga, huku jeshi la polisi likiendelea na uchunguzi wa tukio
hilo.
Tukio hili linakuja ikiwa ni tukio la pili la aina
hiyo kuripotiwa katika Kata ya Old Shinyanga katika kipindi cha hivi karibuni
ambapo mwanafunzi wa kidato cha Nne alifariki kwa kujinyonga.
WANAFUNZI WA KIDATO CHA NNE AFARIKI DUNIA KWA KUJINYONGA OLD SHINYANGA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment