Na Respice Swetu - Misalaba Blog
Idara ya elimu awali na msingi katika halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, imetoa mafunzo ya uimarishaji uongozi kwa maafisaelimu 21wa kata na walimu wakuu 85 wa halmashauri hiyo.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, afisaelimu awali na msingi wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Elestina Chanafi amesema, utoaji wa mafunzo hayo una lenga kuwawezesha washiriki hao kutekeleza kikamilifu majukumu yao.
Amesema kuwa pamoja na kutolewa kwa mafunzo hayo, kutakuwa kunafanyika tathmini ya kiutendaji kwa kila mmoja katika kila kipindi cha miezi mitatu.
"Kila mmoja anatakiwa kutekeleza wajibu na majukumu yake, kutotimiza wajibu ni dhambi sawa na dhambi nyingine", amesema.
Mafunzo hayo ya aina yake yaliyohusisha uwasilishaji wa mada mbalimbali, yalifanyika kwenye ukumbi wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu.
Miongoni mwa mada zilizowasilishwa kwenye mafunzo hayo zilihusu utawala na uongozi, uwekaji wa malengo, stadi za mawasiliano, ufuatiliaji na tathmini na utatuzi wa migogoro.
Sanjari na uwasilishwaji wa mada hizo, Chanafi amewaagiza viongozi hao kuwasainisha mikataba ya utendaji kazi walimu walio katika maeneo yao kama walivyosaini wao ikiwa ni moja ya mikakati ya kuimarisha utendaji kazi na uwajibikaji.
Aidha amemtaka kila mmoja kuhakikisha kuwa, anatekeleza mkakati uliowekwa wa kuwepo kwa chakula cha mchana shuleni, kuondoa tatizo la kutokujua kusoma kuandika na kuhesabu na kukabiliana na utoro pamoja na mdondoko wa wanafunzi kwenye eneo lake.
Awali akifungua mafunzo hayo, kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Vanica Ndelekwa, amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuwalea wanafunzi walio katika shule za msingi kwa maadili mema na kuwajengea ari ya kupenda kuendelea na masomo ya sekondari.
Post a Comment