" SIMULIZI WANAFUNZI WALIOFELI KIDATO CHA PILI

SIMULIZI WANAFUNZI WALIOFELI KIDATO CHA PILI

 


Makundi rika, ukosefu wa malezi kutoka kwa wazazi na umasikini ni miongoni mwa sababu za anguko la wanafunzi wa kidato cha pili kwa matokeo yaliyotangazwa hivi karibuni na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta).

Wakielezea masaibu hayo kupitia mahojiano maalumu na Mwananchi, wanafunzi hao waliofeli mtihani wa kidato cha pili, walisema changamoto hizo zimewachochea kuingia kwenye ukahaba wakiwa na umri mdogo, uuzaji wa dawa za kulevya na kujihusisha na shughuli za muziki wa mitaani ‘vigodoro’.

Hivi karibuni Mwananchi liliripoti habari maalumu ambayo walimu na viongozi wa Shule ya Sekondari Mbagala na Mburahati zilizopo jijini Dar es Salaam walieleza siri ya anguko la wanafunzi katika shule hizo.


Matokeo hayo ya kidato cha pili yalionyesha zaidi ya wanafunzi 400 wa shule za Mbagala na Mburahati wamepata daraja sifuri, jambo lililoibua mjadala miongoni mwa wadau kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.

Wanaofanya ukahaba

Mariam Peter (15) si jina halisi ni miongoni mwa wanafunzi 204 wa sekondari ya Mburahati waliopata daraja sifuri kwenye mtihani wa kidato cha pili, alisema hakupata malezi ya mama yake ambaye ametengana na baba yake.

Mariam alilaani kitendo cha kutokuwa karibu na baba yake ambaye kwa taarifa alizopatiwa anaishi Dar es Salaam lakini hajawahi kuonana naye.

Alisema anguko lake kwenye mtihani huo anaweza kuhusisha na tabia ya mzazi wake kushindwa kuwajibika na kumuonyesha kwamba elimu ni fursa na si mzigo.

Mariam alisema hakuwahi kufikiri angejihusisha na matumizi ya dawa za kulevya au biashara ya ngono ili kupata fedha.

Binti huyo alisimulia alijikuta akijiunga na vikundi vya wanafunzi wanaovuta bangi na kucheza kamari, mambo ambayo yalimfanya aache kuhudhuria darasani.

“Hivi ndivyo nilivyo, mama yangu aliwahi kuniambia nianze kutafuta fedha za kuendeleza maisha yangu,” alisimulia binti huyo kupitia mahojiano kwa simu.

Aliongeza; “kwa sasa nimechoka na maisha haya kutokana na magumu niliyopitia, ni bora nitafute kazi halali ili nijikimu kimaisha, lakini sipo tayari kurudi shuleni.”

Mariam alisema amekuwa akifanya biashara ya ngono kwa muda mrefu, jambo linalomuumiza hadi sasa.

Kuhusu hali ya mtoto huyo, mama yake alipotafutwa na Mwananchi alisema, “achana na maisha yangu. Siko tayari kusema lolote kuhusu binti yangu kwa sababu sasa ni mtu mzima anayeweza kujieleza.”

Ulanguzi wa dawa za kulevya

Katika moja ya migahawa iliyopo Mbagala Rangi Tatu, mwandishi wa habari hizi alikutana na mwathirika mwingine wa matokeo ya kidato cha tatu (jina linahifadhiwa) kwa msaada wa mmoja wa walimu wake.

Wakati wa utambulisho, mwalimu huyo alisema alimkamata kijana huyo akiwa na bangi darasani, lakini akaapa kutomripoti popote, badala yake akaendelea kumshauri ajirekebishe.

“Huyu ni rafiki yetu mwandishi wa habari, zungumza naye bila woga wowote,” mwalimu huyo alimwelekeza mwanafunzi huyo kutoka sekondari ya Mbagala.

Akisimulia maswahibu yake, alisema hadi kuanza tabia hiyo alikuwa akiona namna baba yake anavyovuta na kuuza bangi kwa baadhi ya vikundi eneo la Mbagala na vitongoji vyake.

Alisema wakati mwingine baba yake alikuwa akimtuma kupeleka bangi hiyo kwa baadhi ya wateja wake wakati huo kijana huyo akiwa shule ya msingi.

“Hii ilinipa uzoefu wa biashara na kuzoea wateja wale. Polepole, nilianza kuvutiwa na biashara hii,” alisema.

Mraibu huyo alisema licha ya kuelewa biashara hiyo ni kinyume cha sheria, alipata wakati mgumu kuacha baada ya baba yake kuhamia mkoani Mtwara mwaka 2021.


Kwa mujibu wa kijana huyo, alitumia fedha zinazotokana na biashara hiyo kumtunza mama yake na wadogo zake wanne waliobaki nyumbani bila shughuli ya uhakika ya kuiingizia familia mapato.

“Baba ametuacha kwenye matatizo. Hii inanifanya niendelee kufanya biashara hii katika maeneo maarufu kama Uwezo B na Miti Mirefu.

“Nilifanya mtihani wa kidato cha pili kutokana na shinikizo kubwa kutoka kwa watu katika eneo letu, wakiwemo viongozi,” alisema.

Kijana huyo alisema kuhudhuria kwake shule lengo lilikuwa ni kukutana na wateja wake, akithibitisha kwamba matokeo mabaya aliyoyapata ndiyo aliyoyahitaji.

“Ni bora nisafiri kumfuata baba Mtwara na kujishughulisha na shughuli za kilimo. Nitaachana na biashara hii haramu,” alisema.

Kiongozi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa Mburahati pamoja na mbunge wa Mbagala, Abdallah Chaurembo walisema matukio ya aina hiyo yameporomosha maadili ya wanafunzi na kusababisha kushuka kwa ufaulu wa masomo.

“Watoto maadili yao yameporomoka kwa sababu ya matukio kama haya mitaani,” anasema mmoja wa viongozi hao.

Post a Comment

Previous Post Next Post