Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, kesho Jumatano tarehe 25.01.2023, atawapa daraja takatifu la Ushemasi Mafrateri watatu wa Jimbo, kupitia adhimisho la Misa takatifu ambayo itafanyika katika Kanisa kuu la Mama mwenye huruma Ngokolo mjini Shinyanga.
Kwa mujibu wa Katibu wa Askofu Padre Deusdedith Kisumo, Misa ya utolewaji wa daraja la Ushemasi itaanza saa 4:00 asubuhi.
Mafrateri watakaopewa daraja la Ushemasi ni Emmanuel Ndoma wa Parokia ya Nyalikungu Wilayani Maswa mkoani Simiyu, Sosthenes Ntemi wa Parokia ya Mtakatifu Luka-Bariadi mkoani Simiyu na James F. Mrema wa Parokia ya Mwadui Wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.
Mafrateri hao wanapewa daraja la Ushemasi baada ya kumaliza masomo yao ya Falsafa na Teolojia pamoja na kukamilisha taratibu nyingine zinazotakiwa kwa mujibu wa sheria za Kanisa, ambapo baada ya kipindi kisichopungua miezi sita na bila mapingamizi yoyote, watapewa daraja takatifu la Upadre.
Leo, Askofu Sangu ataongoza Ibada ya Masifu ya jioni, ambayo itafanyika kuanzia saa 11:00 jioni katika Kanisa kuu la Ngokolo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya utolewaji wa daraja la Ushemasi hapo kesho.
Wakati huohuo, kesho Jumatano tarehe 25.01.2023, Askofu Sangu pia atapokea michango ya kuitegemeza Redio Faraja kutoka katika Parokia zote za Jimbo, pamoja kuwasimika rasmi na kuwatuma viongozi wanane wa Kamati tendaji ya Mawasiliano Jimbo ambao wamechaguliwa hivi karibuni, huku watatu miongoni mwao wakiwa ni wa kuteuliwa.
Kamati hiyo pamoja na mambo mengine, itakuwa na Jukumu la kuratibu na kuhamasisha michango ya kuitegemeza Redio Faraja ambacho ndicho chombo kikuu cha Mawasiliano Jimboni, ili iweze kutekeleza kikamilifu majukumu yake katika kusaidia kazi za uinjilishaji na shughuli nyingine za utume wa Kanisa.

Post a Comment