" WAKAZI WA KASULU WAASWA WASIKWEPE KULIPA USHURU.

WAKAZI WA KASULU WAASWA WASIKWEPE KULIPA USHURU.

mkuu wa mkoa wa Kigoma Thomas Andengenye akiweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa nyumba za watumishi wa hospitali hiyo.

Na Respice Swetu
, Misalaba Blog
Mkuu wa mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye amewaasa wakazi wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, kuacha tabia ya kukwepa kulipa ushuru na tozo nyingine.

Hayo ameyasema Jumatano wiki hii
alipokuwa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba tano za watumishi wa idara ya afya wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu zilizojengwa kwenye viwanja vya hospitali ya halmashauri hiyo kwa kutumia pesa za mapato ya ndani.

Andengenye aliyekuwa mgeni rasmi kwenye hafla hiyo amesema kuwa kwa kujenga nyumba hizo, halmashauri ya Wilaya ya Kasulu imetekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan la kila halmashauri kutenga asilimia 40 ya fedha zitokanazo na makusanyo yake  ya ndani kuwarudishia wananchi kupitia miradi inayotoa huduma kwa jamii. 

"Nawapongeza sana halmashauri ya wilaya ya Kasulu kwa kutekeleza agizo hilo, mmewarejeshea wananchi pesa walizozitoa kupitia kwenye tozo, kodi,  ushuru na makusanyo mengine hongereni sana", alisema.

Kutokana na mafanikio hayo, Andengenye amewaasa wakazi wa halmashauri hiyo kuendelea kulipa ushuru na kuachana na tabia ya kukwepa ulipaji wa ushuru na tozo mbalimbali za serikali kwa kuzingatia kuwa manufaa ya tozo hizo yanaonekana.

Akisoma taarifa ya ujenzi wa nyumba hizo, mganga mkuu wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Robert Rwebangila alisema, nyumba hizo zilizokamilika zimegharimu shilingi 291,551,400 ikiwa ni sawa na shilingi 58,310,280 kwa kila nyumba.
 
Aidha kuwepo kwa nyumba hizo kutawezesha kuboresha utoaji wa huduma za afya pamoja na za dharula kwa wakazi wa halmashauri hiyo kwa masaa ishirini na nne.

Kwa upande mwingine nyumba hizo, zitawaongezea morari na ari ya kufanya kazi watumishi wa idara ya afya walio kwenye halmashauri hiyo.


Post a Comment

Previous Post Next Post