mkuu wa mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye (mwenye shati la mikono mirefu) na mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Isaac Mwakisu (mwenye T-shirt) wakipanda miti kwenye eneo la makazi ya watumishi wa idara ya afya wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu.
Na Respice Swetu, Misalaba Blog
Wakazi wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, wametakiwa kupanda miti ya aina mbalimbali kwenye maeneo ya makazi yao.
Kauli hiyo imetolewa kwa pamoja na mkuu wa mkoa wa Kigoma Thomas Andengenye na mkuu wa Wilaya ya Kasulu Isaac Mwakisu walipokuwa wakizungumza na wakazi wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu muda mfupi baada ya kupanda miti katika eneo la nyumba za watumishi wa hospitali ya halmashauri hiyo.
Akizungumza baada ya tukio hilo, Kanali Mwakisu aliyekuwa ameambatana na mkuu wa mkoa wa Kigoma amesema kuwa tukio hilo ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya upandaji miti iliyozinduliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais hivi karibuni.
Amesema kupitia kampeni hiyo, Wilaya ya Kasulu inatarajia kupanda miti ya aina mbalimbali kwenye maeneo ya makazi, yaliyo wazi na katika taasisi.
"Mheshimiwa mkuu wa mkoa, sisi Wilaya ya Kasulu tumekwishajipanga kupanda miti ya aina mbalimbali", alisema Mwakisu alipokuwa akitoa taarifa ya upandaji miti kwa mkuu wa mkoa wa Kigoma.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Kigoma amempongeza Mwakisu na kuwataka wakazi wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kukitumia kipindi hiki kwa kupanda miti.
"Wekeni utaratibu wa kupanda miti kwenye maeneo yenu ili ije kuwasaidia baadaye, upandaji wa miti una manufaa makubwa, itawapatia matunda, itawapatia kuni, itawapatia mbao, italeta mvua na miti mingine ni miti ya kivuli", amesema.
Ameongeza kuwa wananchi wahamasishwe pia kupanda miti kwa kutambulisha alama za mipaka katika nyumba na makazi yao badala ya kutumia vifaa vyenye gharama kubwa.
Akitoa mfano amesema iwapo kila mmoja atapanda miti kuweka mipaka na alama kwenye nyumba na viwanja, atakuwa amepanda miti minne.
Post a Comment