
Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Watoto wawili wa darasa la Nne shule ya msingi
Maganzo Wilaya ya Kishapu wamekutwa wamefariki Dunia kwenye mto unaotiririsha
maji kitongoji cha Mwembeni kijiji cha Masagala kata ya Maganzo.
Akizungumza leo na Misalaba Blog mtendaji wa kijiji
cha Masagala Bwana Kalima Manyesho amesema kuwa tukio hilo limetokea Jumatano
Januari 18,2023 majira ya saa kumi na mbili jion.
Ameeleza kuwa watoto hao ni wakazi wa kitongoji cha
Majengo kata ya Maganzo walikutwa wamefariki Dunia baada ya kuzama kwenye mto
unaotiririsha maji wakiwa wanaogelea kwa kutumia makopo ya ndoo za maji kama
maboya ya kuogelea.
“Nilipigiwa
simu majira ya saa kumi na mbili jioni kwamba watoto hao wamekutwa wakiwa
wamezama kwenye hilo timbwi nikachukua polisi tukaenda kuwatoa tukawapeleka
Hospitali tulipotoka Hospitali tukawapeleka kwa wazazi”
“Lakini
kwa muda huo wa saa kumi na mbili jioni walikuwa tayari wameshatoka shule
nafikiri labda hawakuwa kwenye uangalizi mzuri wa wazazi”.amesema
mtendaji Manyesho
Kwa upande wake mwenyekiti wa kijiji cha Masagala Bwana
Elias Jiganga Masasi amekiri kuwepo kwa tukio hilo huku akiwaomba wazazi
kuwajibika ipasavyo katika suala la ulinzi wa watoto ili kuimarisha usalama wao.
“Taarifa
za watoto hao nilizipokea ni kweli wamefariki jambo hili nalikemea kwa sababu
wazazi huwa tunawaambia mara kwa mara na suala la watoto tulishakataa wasiogelee
kwenye maji wakitoka shule wanatakiwa warudi nyumbani wakatulie hili ni wazazi
tu walishindwa kuwasimamia watoto hao”.amesema mwenyekiti
Masasi
Watoto waliofariki Dunia ni Hamis Ibrahim mwenye
umri wa Miaka kumi (10) na Kadri Rashidi mwenye umri wa Miaka kumi (10) ambao
wote walikuwa wanasoma darasa la Nne shule ya msingi Maganzo Halmashauri ya
Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga.
Mazishi ya Kadri Rashidi yamefanyika siku ya jana
Alhamis huku mazishi ya Hamis Ibrahim yanafanyika leo Ijumaa Januari 20,2023.
Juhudi za kumpata kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga bado hazijafanikiwa.
Post a Comment