" WIKI YA SHERIA SHINYANGA KUADHIMISHWA KWA KUTOA ELIMU

WIKI YA SHERIA SHINYANGA KUADHIMISHWA KWA KUTOA ELIMU

 

Wananchi wa mkoa wa Shinyanga na maeneo jirani, wameshauriwa kutumia kipindi hiki cha maadhimisho ya wiki ya sheria, kwenda kupata elimu kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria, kupitia wataalam ambao watakuwa wakitoa elimu hiyo, katika uwanja wa Zimamoto mjini Shinyanga.

Akizungumza kupitia kipindi maalum kilichorushwa na Redio Faraja, Hakimu mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu mkazi Shinyanga Mh. Asha Hamisi Mwetindwa, amesema kupitia maadhimisho hayo , Mahakama kuu kanda ya Shinyanga kwa kushirikiana na wadau wengine wa Sheria, imeandaa maonesho maaluum ili kutoa nafasi kwa wananchi, waweze kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kisheria ikiwa ni pamoja taratibu za kupeleka mashauri mahakamani.

Mh. Mwetindwa amewaomba wananchi kutumia fursa hiyo, ili kupata elimu ya kutosha ambayo itawasaidia kutatua changamoto mbalimbali za kisheria pindi wanapotafuta haki zao, kwa kuwa watapata nafasi nzuri ya kukutana na wadau wa sheria wakiwemo watumishi wa idara ya Mahakama, Mawakili wa kujitegemea, Jeshi la Polisi, Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU, Ofisi ya Mwendesha mashtaka wa Serikali na Maafisa ustawi wa Jamii.

Kwa upande wake Mwakilishi wa chama cha wanasheria Tanganyika (TLS) katika kanda ya Shinyanga na Simiyu, Wakili wa kujitegemea Chrisantus Chengula, amesema mahitaji ya kuwakilishwa na Mawakili ni makubwa katika uendeshaji wa kesi, kwa kuwa zipo nyaraka muhimu za kisheria ambazo zinatakiwa kuandaliwa kisheria, kabla ya kufikishwa Mahakamani,

Aidha amebainisha kuwa, Mawakili wa kujitegemea kupitia chama chao, wanacho kitengo maalum cha kutoa msaada wa kisheria pasipo malipo, lakini pale tu wanapojiridhisha kuwa mtu huyo anahitaji msaada huo na hawezi kumudu gharama zinazotakiwa.

Kesho  Jumapili tarehe 22.01.2023, Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Shinyanga kwa kushirikiana na wadau wengine wa Sheria, itaungana na Mahakama zote nchini katika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya sheria nchini, ambayo pamoja na mambo mengine, yamelenga kutathmini utendaji wa Mahakama, kupokea maoni na mapendekezo kutoka kwa wadau pamoja na kuelimisha umma kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria.

Maadhimisho hayo yatazinduliwa kwa maandamano maalum ambayo yataanzia katika uwanja wa Mahakama kuu kanda ya Shinyanga, na kuelekea katika uwanja wa Zimamoto ambako elimu kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria itaendelea kutolewa mpaka siku ya kilele tarehe 01.02.2023.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya wiki ya sheria kwa mwaka huu inasema kuwa “UTATUZI WA MIGOGORO KATIKA USULUHISHI KWA AJILI YA KUKUZA UCHUMI ENDELEVU”

Hakimu mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Shinyanga Mh.Asha Hamisi Mwetindwa akiwa katika studio za Redio Faraja kuelezea maadhimisho ya wiki ya Sheria
Mwakilishi wa chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) Kanda ya Shinyanga na Simiyu Chrisantus Chegula akizungumza katika studi za Redio faraja

Post a Comment

Previous Post Next Post