Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, leo tarehe 02.02.2023, anaadhimisha kumbukizi ya miaka minane tangu Baba Mtakatifu farncisco, alipomteua na kumtangaza rasmi kuwa Askofu wa nne wa Jimbo la Shinyanga.
Askofu Sangu ametumia nafasi hiyo kuwashukuru Waamini wote wa Jimbo la Shinyanga, kwa sala na sadaka wanazozitolea kwa ajili yake na Kanisa.
Ameahidi kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu ili kwa baraka zake amuimarishe yeye binasfi, Makleri wote (wenye daraja katika Kanisa) Watawa na Waamini, ili kwa pamoja waweze kulijenga jimbo la Shinyanga listawi kiroho na kimwili, wakiongozwa na fadhila za Imani, matumaini na mapendo.
Askofu Sangu amesema anaikumbuka siku ya terehe 02.02.2015 kuwa ni siku ambayo Mungu alijibu sala na maombi ya muda mrefu Waamini wa Jimbo la Shinyanga, ya kumpata kuhani mkuu na mchungaji mkuu wa Jimbo kupitia nafsi yake, baada ya kuondokewa na mpendwa wao hayati Askofu Aloysius Balina.
“Mungu kwa mapenzi yake alijibu sala na maombi ya Waamini wa Jimbo la Shinyanga ya kumpata Kuhani mkuu na mchungaji mkuu wa Jimbo, baada ya kuondokewa na mpendwa wao Baba Askofu hayati Aloysius Balina, katika nafsi yangu Monsinyori Liberatus T.K. Sangu”
Askofu Sangu aliteuliwa na kutangazwa rasmi kuwa Askofu wa Jimbo la Shinyanga mnamo tarehe 02.02.2015 na Baba mtakatifu Francisco, ambapo aliwekwa wakfu na kusimikwa rasmi mnamo tarehe 12.04.2015.
Mapadre, Watawa, Waamini na watu wenye mapenzi mema, wamemtumia salaam za pongezi na matashi mema katika utume wake wa kulichunga Jimbo la Shinyanga, pale anapofanya kumbukizi hiyo ya miaka minane ya kuteuliwa kwake kuwa Askofu.

Post a Comment