" MWALIMU MAKOYE AONGOZA KIKAO CHA TATHMINI YA MITIHANI MANISPAA YA SHINYANGA

MWALIMU MAKOYE AONGOZA KIKAO CHA TATHMINI YA MITIHANI MANISPAA YA SHINYANGA


Mwalimu Richard Makoye (wa tatu kutoka kulia) akiongoza kikao cha tathmini ya matokeo ya mtihani wa pamoja kwa shule za sekondari za Manispaa ya Shinyanga, kilicholenga kuimarisha taaluma na ufaulu wa wanafunzi.

Na Mapuli Kitina Misalaba

Afisa Elimu Sekondari wa Manispaa ya Shinyanga, Richard Makoye, leo Aprili 21, 2026 ameongoza kikao cha tathmini ya matokeo ya mtihani wa pamoja wa mwezi Aprili, kilicholenga kuchambua maendeleo ya taaluma na kuweka mikakati ya kuboresha ufaulu kwa wanafunzi wa shule za sekondari.

Kikao hicho kilihusisha jumla ya shule 31 za sekondari kutoka Manispaa hiyo, huku washiriki 112 wakijumuisha Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Makamu Wakuu wa Shule pamoja na walimu wa taaluma.

Akizungumza katika kikao hicho, Mwalimu Makoye amesema tathmini hiyo ni sehemu ya juhudi za kuinua kiwango cha elimu kwa kubaini changamoto zilizojitokeza katika matokeo ya mitihani na kuzipatia ufumbuzi wa pamoja.

“Tunataka kuona mabadiliko chanya katika matokeo ya wanafunzi, hivyo ni muhimu kwa walimu na viongozi wa elimu kushirikiana kikamilifu katika utekelezaji wa mikakati iliyowekwa,” amesema Makoye.

Kwa upande wao, Maafisa Elimu Kata wakiongozwa na mwenyekiti Aden Mwakatage pamoja na Grace Mwijarubi wamesisitiza umuhimu wa ufuatiliaji wa karibu kwa walimu na wanafunzi ili kuhakikisha malengo ya kitaaluma yanafikiwa.

Aidha, Mwenyekiti wa Wakuu wa Shule Mkoa, Kisandu Seni, akishirikiana na Katibu Koletha Mgata, wamehimiza nidhamu ya kazi, uwajibikaji pamoja na matumizi bora ya muda wa kujifunza.

Kikao hicho ni sehemu ya mkakati wa Manispaa ya Shinyanga kuimarisha taaluma na kuhakikisha wanafunzi wanapata matokeo bora zaidi katika mitihani yao.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post