" AFISA ELIMU SHINYANGA ATOA WITO WA UMOJA NA AMANI KATIKA KUBORESHA ELIMU

AFISA ELIMU SHINYANGA ATOA WITO WA UMOJA NA AMANI KATIKA KUBORESHA ELIMU

 


Mwalimu Richard Makoye (wa tatu kutoka kulia) akiongoza kikao cha tathmini ya matokeo ya mtihani wa pamoja kwa shule za sekondari za Manispaa ya Shinyanga, kilicholenga kuimarisha taaluma na ufaulu wa wanafunzi.

Na Mapuli Kitina Misalaba

Afisa Elimu Sekondari wa Manispaa ya Shinyanga, Richard Makoye, ametoa wito kwa walimu, wanafunzi na wadau wa elimu kuimarisha umoja na mshikamano ili kuinua kiwango cha elimu na kudumisha amani katika jamii.

Makoye ameyasema hayo leo Aprili 21, 2026 wakati akiongoza kikao cha tathmini ya matokeo ya mtihani wa pamoja wa mwezi Aprili, kilicholenga kuchambua maendeleo ya taaluma na kuweka mikakati ya kuboresha ufaulu kwa wanafunzi wa shule za sekondari.

Kikao hicho kilihusisha jumla ya shule 31 kutoka Manispaa hiyo, kikiwa na washiriki 112 wakiwemo Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Makamu Wakuu wa Shule pamoja na walimu wa taaluma.

Akizungumza katika kikao hicho, Makoye amesema mafanikio ya elimu hayawezi kupatikana bila ushirikiano, akisisitiza kuwa walimu wanapaswa kufanya kazi kwa umoja, nidhamu na kujituma ili kuwajengea wanafunzi msingi imara wa kitaaluma na maadili mema.

“Tunataka kuona mabadiliko chanya katika matokeo ya wanafunzi, hivyo ni muhimu kwa walimu na viongozi wa elimu kushirikiana kikamilifu katika utekelezaji wa mikakati iliyowekwa,” amesema Makoye.

Makoye pia ametoa rai kwa walimu kuendelea kuwa mlezi bora wa wanafunzi si tu katika taaluma bali pia katika kuwajenga kiakili na kimaadili, ili waweze kuwa raia wema watakaolinda amani ya taifa.

Kwa ujumla, kikao hicho kimeweka msisitizo katika kujenga mshikamano miongoni mwa wadau wa elimu, kikilenga kuhakikisha kuwa mazingira ya kujifunzia yanakuwa ya amani, salama na yenye tija kwa maendeleo ya wanafunzi na taifa kwa ujumla.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post