Askofu wa Kanisa katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, kesho alhamisi tarehe 02.02.2023, ataadhimisha kumbukizi ya miaka 8 tangu Baba Mtakatifu Francisco alipomteua na kumtangaza rasmi kuwa Askofu wa Shinyanga.
Askofu Sangu aliteuliwa na kutangazwa kuwa Askofu wa nne wa Jimbo la Shinyanga mnamo tarehe 02.02.2015, kufuatia kifo cha aliyekuwa Askofu wa tatu wa Jimbo la Shinyanga hayati Aloysius Balina.
Baada ya kuwekwa wakfu na kusimikwa rasmi mnamo Aprili 12.2015, aliahidi kuendeleza mema yote yaliyoaasisiwa na watangulizi wake, kwa ajili ya ustawi wa Jimbo la Shinyanga na Kanisa kwa ujumla.
Askofu Sangu anaendelea kufanya juhudi mbalimbali za kuimarisha moyo imani na majitoleo kwa waamini, kusogeza huduma za kiroho kwa waamini, kuboresha huduma za uinjilishaji na huduma za jamii zinazofanywa na Kanisa.
Anaadhimimisha kumbukizi ya miaka minane ya kuteuliwa kwake huku kukishuhudiwa mafanikio kadhaa kupitia nafsi yake, ambayo ni pamoja na ongezeko la Waseminari wakubwa kutoka 24 mwaka 2015, hadi kufikia 76 mwaka huu 2023.
Askofu Sangu alianza utume wakati jimbo la Shinyanga likiwa na Parokia 26 pekee, ambapo kupitia kampeni yake ya kusogeza huduma za kiroho kwa waamini, amefanikiwa kuanzisha jumla ya Parokia mpya 11 za Ngulyati, Nindo, Old Shinyanga, Mhunze, Ndala, Mt.Luka Bariadi, Kitangili, Bukundi, Lubaga, Maganzo na Luguru na kulifanya Jimbo kuwa na jumla ya Parokia 37 mpaka hivi sasa.
Pamoja na mambo mengine, Askofu Sangu pia ameanzisha Shirika jipya Kijimbo la watawa wa kike la Mtakatifu Bikra Maria Mama mwenye huruma, na ameshirikiana na watu wenye mapenzi mema kukifanyia maboresho chuo cha Makatekista kilichopo Mipa wilayani Kishapu.
Kupitia kaulimbiu yake ya Upendo ni tunda la roho Mtakatifu, Askofu Sangu pia amekuwa mdau muhimu katika kuhamasisha umoja, amani na mshikamano kwa watanzania, pamoja na kuongoza juhudi za kupinga ukatili kwa wanawake na watoto kupitia shughuli zake za kichungaji.
Kupitia maadhimisho hayo, Mapadre, waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanamtakia Askofu Sangu matashi mema katika utume wake wa kuliongoza na kulichunga Jimbo Katoliki Shinyanga.
CHINI NI PICHA ZINAZOMWONYESHA ASKOFU SANGU AKIWA KATIKA UTEKELEZAJI WA SHUGHULI MBALIMBALI ZA KITUME JIMBONI













Post a Comment