Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama imesema Serikali inatumia wastani wa Sh15.54 milioni kwa siku kuwapatia huduma mbalimbali za msingi mahabusu na wafungwa wanaotokana na makosa ya uhamiaji haramu.
Hayo yamesemwa leo na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Vita Kawawa wakati akisoma taarifa ya shughuli za kamati hiyo ya Bunge kwa kipindi cha kati ya Februari 2022 hadi Januari 2023.
Kawawa amesema taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani zilionesha kuwa kwa kipindi cha Septemba hadi Desemba, 2022 jumla ya wahamiaji haramu 7,493 walikamatwa katika maeneo mbalimbali nchini.
“Kamati ilibaini kuwa katika kipindi cha Septemba hadi Desemba, 2022, katika magereza mbalimbali nchini kulikuwa na wafungwa na mahabusu wahamiaji haramu wapatao 3, 108,”amesema.
Amesema idadi hiyo imeongezeka kwa asilimia 93 ikilinganishwa na wahamiaji haramu 1,608 waliokuwepo magerezani katika kipindi kama hicho mwaka 2021.
Kawawa amesema uwepo wa wahamiaji haramu magerezani, unaigharimu Serikali kiasi cha wastani wa Sh15.54 milioni kwa siku katika kuwapatia huduma mbalimbali za msingi.
Amesema ikiwa hali itabakia kama ilivyo Serikali inatumia Sh5.673bilioni kwa mwaka kuwatunza wafungwa na mahabusu hao.
Amesema kiasi hicho cha fedha kinachotumika kuwatunza wafungwa na mahabusu hao kingeweza kununua madawati 81, 030 kwa kila dawati kugharimu Sh70, 000.
Amesema Serikali pamoja na mamlaka zije na mpango mkakati wa muda mrefu na unaotekelezeka utakao hakikisha kwamba, nchi yetu haindelei kuwa na wahamaiji haramu.
Chanzo - Mwananchi
Post a Comment