Kufuatia kutolewa kwa vigezo 19 vya kupima utendaji kazi kwa walimu wa shule za msingi nchini, idara ya elimu awali na msingi katika halmashauri ya Wilaya ya Kasulu imewataka walimu kuvitekeleza vigezo hivyo.
Maagizo hayo yametolewa katika nyakati tofauti na maafisaelimu wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu walipokutana na walimu wa halmashauri hiyo wakati wa kuwawasilishia vigezo hivyo.
Walisema kuwa, vigezo hivyo ni muhimu kwa kuwa vitaiwezesha pia halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kufanya vizuri kwenye mitihani ya upimaji wa darasa la nne na wa kuhitimu darasa la saba matokeo ambayo hayakuwa mazuri.
Akitoa taarifa ya matokeo ya mitihani hiyo, afisaelimu taaluma wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Joseph Maiga alisema halmashauri ya Wilaya ya Kasulu imekuwa ya tano kati ya halmashauri nane kwenye mtihani wa kuhitimu darasa la saba na ya saba katika mtihani wa upimaji wa darasa la nne.
"Matokeo hayo sio mazuri kwetu sisi na hata kitaifa hayakuwa mazuri, na kutokana na matokeo hayo Ofisi ya Rais Tamisemi na wizara ya elimu wamefanya tathmini wakaja na vigezo 19 vya upimaji vitakavyosaidia kupandisha ufaulu huo", alisema.
Miongoni mwa vigezo alivyovitaja
Maiga vilivyowekwa kutokana na anguko hilo ni pamoja na shule kufanya tathmini ya mitihani kila baada ya matokeo, kudhibiti utoro na mdondoko wa wanafunzi.
Kuhusu ufaulu wa wanafunzi, vigezo hivyo vinawataka walimu kufaulisha darasa la saba kwa asilimia 95 huku wanafunzi wa darasa la nne wakitakiwa kufaulu kwa asilimia 100.
Vigezo hivyo vinaitaka pia shule kuweka mpango mkakati wa kuhakikisha kuwa watoto wote wa darasa la kwanza wanajua kusoma, kuandika na kuhesabu.
Aidha kupitia vigezo hivyo, wanafunzi wa darasa la tatu wanatakiwa kupata umahiri wa stadi za somo la Kiingereza.
Kupitia vigezo hivyo, walimu wametakiwa pia kushirikiana na kamati za shule kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata chakula cha mchana wawapo shuleni.
Akizungumza na walimu wa kata ya Nyamidaho katika kikao kilichofanyika kwenye shule ya Msingi Mvugwe, afisaelimu wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu Elestina Chanafi alisema ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha anatekeleza vigezo hivyo.
"Baada ya kuwasilisha vigezo hivi tutaanza kupita kuona utekelezaji wake, tumepewa siku mbili tu za kukaa ofisini na siku zinazobaki tutakuwa shuleni", amesema.
Ameongeza pia kuwa, walimu wanatakiwa kuiona kazi ya ualimu kuwa ndio kipaumbele cha kwanza kwa kujituma na kuacha alama kwenye maeneo yao,
"msichanganye muda wa kazi na mambo mengine na anayeona biashara inalipa kuliko kazi aache kazi", alisema.
Katika hali inayoonesha kuweka msisitizo, Chanafi alirudia
kauli yake kuwa mwaka huu afe kipa afe beki kauli aliyoitoa siku chache zilizopita alipokuwa akizungumza na walimu pamoja na wadau wa kata ya Buhoro.
Kikao hicho kilihitimisha mzunguko wa kuzungumza na walimu pamoja na wadau wengine kuhamasisha utekelezaji wa vigezo hivyo na kuwafikiwa walimu wa shule zote 85, viongozi wa kamati za shule, wawakilishi wa madhebu ya dini, watendaji wa vijji pamoja na wa kata 21 za halmashauri ya Wilaya ya Kasulu
Baadhi ya walimu na wadau mbalimbali (pichani) wakisikiliza vigezo vya kupima utendaji kazi.
Post a Comment