
Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Kwa wale waliopata kusoma historia au kusikia hadithi za makabila, hasa ya Wasukuma na Wanyamwezi, hawakukosa kusikia habari ya Ng’wanamalundi.
Misalaba Blog imefika na kuzungumza na baadhi ya jamii ya eneo hilo ambao wameeleza kuwa kaburi la Ng’wanamalundi limejengwa kupitia uongozi wa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Lengo la serikali lilikuwa ni kutambua mchango wa Ng’wanamalundi kupitia uwezo wake aliokuwa nao ambapo inasemakana ni kweli alikuwa namchango mkubwa katika jamii.
Mtu huyo aliyewahi kuutingisha utawala wa Wajerumani, alizaliwa katika ukoo wa kawaida akiwa mcheza ngoma mashuhuri, mwaka wa kuzaliwa 1840 akiwa katika kijiji cha Seke Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga alifariki dunia Februari 2 mwaka 1936.
Katika makala hii usahihi wa historia yake unaelezwa kuwa watu wengi walikuwa wakimjadili kwa maoni tofauti, wengine wakimsifu kama shujaa huku wengine wakihusisha uwezo wake na nguvu za giza.
Jina lake halisi halikuwa Ng’wanamalundi bali lilikuwa Igulu Bugomola, ambaye alizaliwa katika Kijiji cha Mwakubunga Nera wilayani Kwimba mkoani Mwanza.
Ng’wanamalundi alikuwa mtoto pekee wa kiume na wa mwisho kati ya wanne, kwa baba yake Bugomola na mama yake, Ngolo Igulu.
Igulu (Ng’wanamalundi), alikuwa na tabia ya uzururaji tangu utotoni na mara nyingi haikuwa rahisi kumkuta nyumbani alikuwa mashuhuri kutokana na umahiri wake wa kucheza ngoma na mara nyingi alipokuwa akitembea mitaani alifuatwa na kundi kubwa la watoto.
Hali ya kuchukiwa kwa Ng’wanamalundi ilienea pale kijijini kiasi cha kuanza kumkebehi, hasa kutokana na umbo lake refu na miguu yake myembamba kuanzia magotini hadi kwenye makanyagio, ikiwa mirefu kuliko kawaida.
Hali hiyo ilisababisha kumdhihaki na kumwongezea chuki zaidi kwa wanakijiji wa eneo hilo waliodiriki kumtukana kwa lugha ya Kisukuma hapo ndipo ukawa mwanzo wa kufutika kwa jina la Igulu na kuwa Ng’wanamalundi, jina ambalo lilitokana na urefu wa miguu yake na kila kona walimuita hivyo.
Kadiri siku zilivyosonga mbele Ng’wanamalundi alizidi kujiimarisha katika kikundi chake cha ngoma ambayo ilivuta vijana wengi, pia baadaye ilitumika kama jeshi la kukodiwa na Watemi inapotokea vita.
Pamoja na wazazi kumchukia sana, lakini vijana walimpenda na kikundi chake kikubwa cha ngoma kilipendwa na kutumika katika sherehe mbalimbali kwenye familia za Kitemi za wakati huo.
Ng’wanamalundi na wenzake wawili walikwenda kwa bibi kizee mmoja kutafuta dawa itakayowasaidia katika shughuli zao za kucheza ngoma, ambapo bibi kizee huyo alikubali kuwasaidia.
Imeelezwa kuwa baada ya kusimama aliamuru kila mmoja achimbe shimo lenye urefu hadi kiunoni, na baada ya kukamilika kwa mashimo hayo aliwaambia wakusanye kuni na kuzitumbukiza.
Baada ya kazi hiyo kukamilika walipekecha moto na kuziwasha zile kuni na moto uliposhika kasi aliwachukua wale vinyonga watatu na kuwawekea dawa mdomoni na kisha aliwatupia ndani ya moto huo, wakateketea wote.
Ngw’anamalundi alikimbia akapanda juu ya mti, kifaru alifika kwenye shina la mti na kuanza kuliparua kwa hasira na baadaye aliondoka kabla hajafika mbali alimuona yule bibi kizee akikutana na faru huyo.
Ng’wanamalundi alishuhudia kifaru akimrarua rarua bibi kizee mpaka akafa, kisha kifaru alitoweka kusikojulikana huku akimuacha Ng’wanamalundi asijue la kufanya juu ya mti.
Ng’wanamalundi baada ya muda alishuka juu ya mti na kwenda kwenye maiti ya yule bibi kizee, akaamua aibebe mgongoni airejeshe nyumbani, lakini kabla hajafika mbali alisikia sauti ikisema, “Igulu bajahe abiyo akiwa na maana Igulu wenzako wamekwenda wapi”.
Sauti hiyo ilimshtua Ng’wanamalundi ambaye alimshusha bibi kizee mgongoni mwake na akashangaa kumuona akiwa hai asiyekuwa na jeraha lolote, kama alivyokuwa baada ya kushambuliwa na faru.
“Igulu tujage ahante ugo waliwalinaga, akiwa na maana Igulu twende kwenye mti uliokuwa umepanda, Ng’wanamalundi aliongozana na bibi kizee huyo mpaka kwenye ule mti aliyachukua magamba ya mti yaliyokuwa yameparuliwa na faru,”
Baada ya zoezi hilo kukamilika bibi kizee huyo alimtengenezea dawa aliyokuwa akihitaji, na kisha Mwanamalundi alirejea kwao kuendelea na shughuli zake za ngoma aina ya Kahena, ambayo mpaka leo inaendelea kwa baadhi ya maeneo jina lingine ni Wigashe.
Ng’wanamalundi akiwa katika harakati zake za kujiimarisha katika masuala ya dawa zake za ngoma, alienda kuchimba kwenye pori la Mwandutu huko wilayani Maswa sasa ni Wilaya ya Kishapu, ambalo lilikuwa katika miliki ya Mtemi Chalya.
Imeelezwa kuwa baada ya kufika katika pori hilo akiwa na wafuasi wake wakiendelea kuchimba dawa, ghafla alitokea Mtemi Chalya na kumuuliza; “Ubebe nani wakuwilaga kwiza ngh’wiporu lyane” akiwa na maana; “Wewe nani amekuambia kuja kwenye pori langu?”
Mwanamalundi alimjibu; “ Ubebe ulintemi wa banhu pye nu nene nding’wenekele wa maporu pyee.” Akiwa na maana “Wewe ni Mtemi wa watu wote na mimi ni mmiliki wa mapori yote”. Kauli hiyo ilimuudhi Mtemi Chalya.
Anasema, kufuatia kauli hiyo Mtemi Chalya aliita jeshi lake kwa lengo la kuja kumkamata, lakini walishangaa baada ya kufika katika eneo waliloelezwa na Mtemi wao kuwa Ng’wanamalundi anatakiwa kukamatwa na kuuawa, lakini walishindwa baada ya kukuta simba wengi sana.
Jeshi hilo na Mtemi ilibidi kukimbia kujiokoa kwani simba hao walianza kuwashambulia, wengine walitawanyika ovyo na baadhi yao wachache tu ndiyo walionusurika.
Lakini cha kushangaza walipofika walimkuta Ng’wanamalundi na wafuasi wake wakimalizia kula chakula nyumbani kwa Mtemi Chalya, ambaye hata yeye alichanganyikiwa na kushindwa kuongea lolote.
Ng’wanamalundi baada ya kumaliza kula chakula kwa Mtemi Chalya aliondoka na wafuasi wake na akapitia kwenye lile pori akachimba dawa zake na kuondoka kwenda kuendelea na maisha yake.
Katika ngoma zake; Ng’wanamalundi alikuwa na tabia ya kuwatahadharisha mashabiki wake kuacha kwenda wakiwa wamejipaka dawa yoyote ile, anasema. Aliwaambia: “Bing’we akwiziza munho wibilaga bugota bosebose ulu kutora akotora henaha,ulo nsabo akupandika heneha.”
Kauli hiyo ilikuwa na maana nyie asije mtu amejipaka dawa yoyote hapa kama ni kuoa, ataoa hapahapa kama ni mali atapata hapahapa, hata hivyo kuna wale walipuuza kauli hiyo kwa kuja wamejipaka dawa kwa lengo la kujipima uwezo wa dawa zao. Lakini hawakufanikiwa na badala yake walikufa.
Akiwa anaendelea na ngoma yake wananchi wa Kijiji cha Sekke waliibiwa ng’ombe wengi sana na watu kutoka Kabila la Wamasai ambao walienda kuwahifadhi katika Pori la Mwanima karibu na Kijiji cha Bubiki.
Ng’wanamalundi na kikosi chake waliondoka Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza na kuelekea Sekke wilayani Kishapu mkoani Shinyanga kwa lengo la kusaidia kuzikomboa ng’ombe zilizoibwa. Hata hivyo kabla hawajafika uwanja wa vita, Ng’wanamalundi alifanya utabiri wake uliotokana na nguvu ambazo alizipata kutoka kwa Bibi Kizee wa porini.
Aliwaambia kuwa kabla ya vita, itatokea mvua kubwa sana na ikikatika watakuja ndege hai aina ya mwewe watakaokuwa wanazungukazunguka kwenye zile ng’ombe na hapo sasa wafuasi wake wakate miti mifupi mifupi (Lubugu).
Utabiri huo ulitimia, kwani mvua ilinyesha kubwa sana na baada ya kukatika wale mwewe walijitokeza wengi sana wakawa wanazunguka kwenye zile ng’ombe na ndipo yale mapigano ya Wamasai na wafuasi wake yalipoanza.
Aliwaeleza kuwa baada ya kuwa na fimbo ya Lubugu wale wenye upinde na mishale watakaa nyuma na kazi yao watakuwa wanazipiga zile ngao za Kimasai na zikidondoka chini ndipo wenye pinde na mishale waanze kushambulia.
Mwanamalundi alipigana hiyo vita ya Wamasai mpaka akazirejesha zile ng’ombe na aliwatokomeza Wamasai mpaka kwenye mpaka wa Mto Manonga unaotenganisha Tinde Shinyanga na Nzega mkoani Tabora.
Hapo ndipo ilibainika Wamasai hao walikuwa wametumwa kuiba ng’ombe Usukumani na Mtemi Tinginya wa Busongo Nzega, ambapo baada ya vita hiyo Ng’wanamalundi na kundi lake walirudi Sekke na kupewa jina la Kishosha Mang’ombe tafsiri ikiwa ni mrudisha ng’ombe. Baada ya vita hiyo Ng’wanamalundi alirudi nyumbani kwao wilayani Kwimba kuoa, lakini bahati mbaya ilimkuta, kwani kila mke aliyejifungua, mtoto alikufa.
Baba yake Bugomola akaenda Ntuzu kwa sasa Bariadi kufanyiwa tambiko kuhusu uzazi kwa mwanaye. Akiwa huko Ntuzu, Bugomola alielezwa mwanaye Ng’wanamalundi hatapata mtoto kwa wake zake alionao.
Hivyo aoe msichana atakayempata upande wa Mashariki ambaye atakuwa akiitwa Nkamba na atazaa watoto watatu; wa kwanza ataitwa Sitta, wa pili Ngassa na wa tatu Marieta.
Baada ya kurudi Bugomola, haikumchukua muda mwanaye Ng’wanamalundi akapata msichana akaoa na akaendelea na shughuli yake ya kuendesha kikundi cha ngoma.
Ng’wanamalundi kuwekwa kizuizini Akiwa anaendelea na ngoma zake katika maeneo ya Kanda ya Ziwa, siku moja yeye na kikundi chake walipokuwa wakiburudisha katika maeneo ya Bukumbi mkoani Mwanza, wafuasi wake walipumzika kwenye mti mkubwa ambapo pia kilikuwa Kituo cha Wajerumani, Ng’wanamalundi aliwaambia wafuasi wake waondoke waende kwenye ngoma, wafuasi wake waligoma wakadai wanapumzika kwenye kivuli hicho ili wavute sigara.
Baada ya kuwabembeleza vya kutosha akabaini hawataki kumsikiliza ndipo alipounyooshea kidole ule mti akisema “Ngh’walemelaga hanti gunugo aliyo gumaga,” akiwa na maana “Mmekatalia kwenye mti huo huku ukiwa umekauka.” Ghafla mti huo wote ulikauka.
Kuona hivyo wafuasi wake wakaondoka wote kwenye huo mti wakaenda kuendelea na ngoma yao ambayo walicheza katika eneo la Bukumbi na Busagara karibu na Mji wa Mwanza na walipomaliza walirejea Kwimba.
Akiwa Kwimba alicheza ngoma moja na Gindu Nkima, ngoma hiyo ilikuwa ngumu kwake ilichezwa sehemu za Mwanagwa.
Baada ya kuwa amezidiwa Ng’wanamalundi, wapishi wake walimfuata na kumtaka awasaidie namna ya kupata kuni za kupikia. Kutokana na uharaka aliokuwa nao Ng’wanamalundi alielekeza kidole chake kwenye miti ya minyaa iliyokuwa mbele yake huku akisema “Batemagi pye abenababa mkazugile,” akiwa na maana “Yakateni yote haya mkapikie.”
Baada ya kauli hiyo minyaa yote ilikauka na kuwa kuni na wafuasi wake walikata wakaenda kupikia chakula akiwa katika ngoma hiyo wakati huo barabara ya kutoka Shinyanga kwenda Mwanza ilikuwa inachongwa na manamba waliokuwa wakikamatwa na Wajerumani kwa ajili ya kazi hiyo, Gavana wa Kijerumani wa eneo la Mwanza alipita eneo hilo akiwa amepanda punda alikuta kazi imesimama, alipohoji kwanini kazi imesima alielezwa wananchi wote wamekwenda kwenye ngoma ya Ng’wanamalundi.
Kitendo hicho kilimchukiza sana Mjerumani huyo, ambaye aliondoka akaenda Mwanza na baada ya siku mbili walikuja askari waliomkamata Ng’wanamalundi na kumfunga mnyororo na watuhumiwa wengine walipelekwa Mwanza na kuwekwa gerezani.
Kosa hilo kwa utawala wa Ujerumani lilihesabiwa kuwa ni uhaini wa kupinga utawala wao hivyo alitakiwa kupewa adhabu ya kunyongwa. Kabla hajapelekwa Mwanza, kwa kuwa ilikuwa ni safari ya kwenda kunyogwa, alipelekwa nyumbani kwa wazazi wake kuaga.
Alipofika nyumbani kwao alimpa mama yake shoka aliloliweka pembezoni mwa ukuta chumbani na maziwa, huku akitoa maelekezo. “Mayu imbasa yeneye ulu yulina ng’wigulya mumhonatwalwa ulu yika hase mumhonashoka amabele genaya ulu guganda mumhonacha, ulu gita lububhi mumhonasata.” akiwa na maana hii shoka ikipanda juu basi nitakuwa nimepelekwa ikishuka chini nitakuwa nimerudishwa.”
Ng’wanamalundi aliendelea kumpa maelekezo mama yake kuwa haya maziwa yakiganda atakuwa amekufa na pindi yakipata utando atakuwa anaumwa, baada ya maelezo hayo Ng’wanamalundi alipelekwa Mwanza gerezani ambako alikutana na Mtemi Makongoro wa Mwanza.
Siku iliyofuata walitolewa wote ambapo walikutana pia na mganga aliyemtabiria kuzaa watoto watatu ambaye naye alikuwa amekamatwa kwa kosa la kupiga ramli iliyosababisha mauaji ya kishirikina.
Asubuhi kila mmoja alisomewa mashtaka yake ambapo Ng’wanamalundi alisomewa mashtaka matatu, shtaka la kwanza kuukausha mti uliokuwa ukitumiwa na maofisa wa utawala wa Wajerumani kama kituo cha kupumzikia huko Bukumbi Mwanza.
Shtaka la pili kuwatungia na kuwaimbia nyimbo mbaya Wajerumani na la tatu ni kukwamisha ujenzi wa Barabara ya Mwanza kwenda Shinyanga.
Ng’wanamalundi alidaiwa kuchezesha ngoma eneo la Mwanangwa hali iliyosababisha wafanyakazi wa manamba waliokuwa wakilima barabara hiyo kuacha na kwenda kuangalia ngoma yake hali iliyowachukiza Wajerumani.



Holo Bunzali ambaye ni ndugu yake na Ng'wanamalundi wakati akiwa ni mmoja ya waliopata nafasi ya kuzungumza na Misalaba Blog














Makaburi ya watoto wa Ng'wanamalundi .TAZAMA PICHA ZOTE HAPA CHINI















TAZAMA VIDEO

Post a Comment