Wakristo wametakiwa kuwa na moyo wa msamaha, hatua ambayo italeta maelewano katika maisha yao ya kila siku.
Hayo ni kwa mujibu wa mafundisho ya Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga, Mhashamu Liberatus Sangu, ambayo ameyatoa leo kupitia ibada ya Ijumaa kuu iliyofanyika katika Kanisa kuu la Mama mwenye Huruma Ngokolo mjini Shinyanga.
Askofu Sangu amesema ndoa na familia nyingi zimevurugika kutokana na kukosa moyo wa msamaha.
Askofu Sangu amewataka Wakristo kuitafakari kwa kina sala ya Baba yetu na kuipa uzito unaostahili, hasa kwenye eneo linalohusu msamaha.
Amezitaja faida za kujenga moyo wa kusameheana na kuachana na hali ya kulipiza kisasi ndani ya familia na jamii kuwa ni pamoja na kuimarika kwa hali ya amani, umoja, upendo na mshikamano.
Askofu Sangu ametumia maadhimisho ya ibada ya Ijumaa kuu kuwaalika Wakristo wote kutafakari mateso na kifo cha Kristo msalabani kwa kutobaki katika maisha ya dhambi pamoja na kuwa watu wa msamaha wakiiga mfano wa Mtakafifu Yohane Paul II (Papa) aliyemsamehe na kwenda kumtembelea gerezani mtu aliyetaka kumuua kwa kumpiga risasi.
Leo Ijumaa tarehe 07.04.2023, wakristo kote duniani wameungana kuadhimisha kumbukumbu ya mateso na kifo cha Yesu Kristo Msalabani, ambaye alishinda mauti na kufufuka siku ya tatu.
Post a Comment