" HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU YAENDELEA KUNG'ARA KATIKA UTOAJI WA MIKOPO YA ASILIMIA KUMI.

HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU YAENDELEA KUNG'ARA KATIKA UTOAJI WA MIKOPO YA ASILIMIA KUMI.


Kufuatia maelekezo ya serikali kuzitaka mamlaka za halmashauri nchini kutenga asilimia kumi ya fedha zitokanazo na mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma imeendelea kuwa kinara wa kutekeleza agizo hilo.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kukabidhi pikipiki 15  kwa kikundi cha vijana cha "Twaweza" kutoka katika kata ya Makere, mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Eliyah Kagoma amesema kuwa, halmashauri hiyo itaendelea kutoa mikopo kwa vijana na kwa makundi mengine.

Kagoma amewaambia vijana waliopata mkopo wa pikipiki hizo kuwa, wanatakiwa kutumia nguvu, akili na kuwa wabunifu katika kazi wanayokwenda kufanya ili kurejesha fedha zikizotumika kununua pikipiki hizo.

"Hampewi bure hizi pikipiki, mnatakiwa mkazitumie kama mtaji utakaowawezesha kupata pesa za kurejesha gharama zilizotumika kununua pikipiki hizo na kujijengea imani na uaminifu kwa serikali," amesema.

Aidha amewataka vijana hao kuepuka kuzitumia pikipiki hizo katika matumizi maovu yakiwemo ya kuchepusha mapato ya halmashauri na kusafirisha wahalifu na badala yake waisaidie halmashauri kutoa taarifa watakapoona kuna uchepushaji wa mapato kwa kuzingatia kuwa kwa  kupewa mkopo huo, na wao sasa ni sehemu ya halmashauri.

"Pesa za mkopo wa kununulia pikipiki hizo zimetokana na makusanyo ya ndani hivyo mkiona watumishi wa halmashauri wanakuja kukusanya mapato, ushuru na tozo mbalimbali toeni ushirikiano, huko ndiko zilipotoka pesa zilizonunua pikipiki hizo" amewaambia.

Kagoma amewaasa pia vijana hao kuzingatia sheria na kujiepusha na uendeshaji wa mwendo wa kasi watakapokuwa wakitumia pikipiki hizo.

Akimkaribisha mwenyekiti wa halmashauri kukabidhi pikipiki hizo, kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu Ndelekwa Vanika amesema, mikopo hiyo inatokana na uongozi mzuri wa serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuwataka vijana hao kuishukuru serikali kwa mambo mazuri yanayofanyika.

Akitoa maelezo kuhusu mikopo hiyo, Afisa Maendeleo ya jamii wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Victoria Makyao amesema, katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2022 na 2023, halmashauri ya Wilaya ya Kasulu imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni mia mbili na laki nane.

Amefafanua kuwa kati ya fedha hizo, shilingi milioni tisini na tano zimetokana na makusanyo ya mapato ya ndani huku shilingi milioni mia moja kumi na tatu zikiwa zimetokana na marejesho ya mikopo hiyo.

Ameongeza kuwa kupitia pesa hizo, jumla ya vikundi 24 vimenufaika na kuvitaja vikundi hivyo na mikopo waliopata kuwa ni vikundi 13 vya wanawake vilivyopata shilingi milioni themanini na saba, vikundi 8 vya vijana vilivyopata shilingi milioni tisini na tano, huku vikundi 3 vya watu wenye ulemavu vikiwa vimepata mikopo yenye thamani ya shilingi milioni ishirini na sita.

Post a Comment

Previous Post Next Post