" WANANCHI WATAKIWA KUFUATA SHERIA NA TARATIBU KIPINDI CHA SIKUKUU, KAMANDA MAGOMI APIGA MARUFUKU DISKO TOTO

WANANCHI WATAKIWA KUFUATA SHERIA NA TARATIBU KIPINDI CHA SIKUKUU, KAMANDA MAGOMI APIGA MARUFUKU DISKO TOTO

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi, amepiga marufuku kumbi za starehe kuandaa Disko kwa watoto maarufu kama Disko toto, katika kipindi chote cha sikuu ya Pasaka.
Akizungumza na waandishi wa Habari amebainisha kuwa, wamiliki wa kumbi za sterehe watakaopuuza agizo hilo watachukuliwa hatua kali za kisheria na kwamba, wazazi na walezi wanapaswa kuhakikisha usalama watoto wao kwa kuwatowaruhusu kwenda kwenye kumbi za starehe.
Kamanda Magomi pia amewataka wamiliki wa kumbi za starehe kuzingatia sheria, kwa kuhakikisha wanafunga shughuli zao ifikapo saa 6:00 usiku, isipokuwa tu kwa wale watakaokuwa na vibali maalum.
Wakati huohuo, Kamanda Magomi amewatahadharisha wananchi kutotumia sherehe za Pasaka kama fursa ya kufanya uhalifu, huku akiwataka madereva wa vyombo vya moto kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali, ikiwa ni pamoja na kutoendesha vyombo hivyo huku wakiwa wamelewa.
Amesema Jeshi la Polisi limejipanga kukabiliana na uhalifu wowote utakaojitokeza wakati wa sikukuu ya Pasaka, na amewaomba wananchi kushirikiana na jeshi hilo kwa kutoa taarifa mapema pale wanapoona viashiria vya uhalifu.
Sherehe za Pasaka ambazo huadhimishwa na Wakristo kote Duniani kama kumbukumbu ya kufufuka kwa mkombozi wao Yesu Kristo siku ya tatu baada ya kuteswa na kufa Msalabani, kwa mwaka huu 2023, zitaanza usiku wa Jumamosi tarehe 08 hadi Jumapili tarehe 09.04, 2023.
Sherehe hizo pia huhitimisha kipindi cha siku 40 za kufunga na kujiweka karibu zaidi na Mwenyezi Mungu, kinachojulikana kama Kwaresima.

Post a Comment

Previous Post Next Post