Mwanaume mmoja anayefahamika kwa jina la Ally Hamis mwenye umri wa Miaka 48 amekutwa amejinyonga hadi kufa ndani ya Nyumba yake katika kijiji cha Itwangi Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
Misalaba Blog imetapa taarifa hizo kutoka kwa Mwenyekiti wa kijiji cha Itwangi Bwana Kisendi Lubinza ambaye amesema tukio hilo limetokea leo April 8,2023 majira ya asubuhi baada ya familia kumkuta marehemu amejinyonga ndani ya Nyumba yake.
Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa marehemu Ally Hamis ameacha wosia ambapo ameandika ujumbe kwa kuorodhesha gharama ya madeni anayodaiwa huku akiwaomba ndugu zake kuyalipa madeni hayo.
“Muda was aa nne asubuhi nilipata taarifa kuwa Ally Hamis amejinyonga kwanza sikuamini badaye akanipigia Mheshimiwa Diwani ikabidi niende kwenye hiyo Familia ni kweli nikalikuta tukio hilo nilipouliza wakasema tayari wameshatoa taarifa kituo cha Polisi”.amesema Mwenyekiti wa kijiji Bwana Lubinza
“Kuna wosia ameandika na ameorodhesha madeni yake yote akasema ndugu wasiache kuyalipa aliandika deni la Baskeli yake alikuwa anadaiwa elfu arobaini (40000), kuna Baba yake mdogo alipwe laki tatu na mwingine alipwe debe moja la Mahindi badaye kwenye wosia wake akasema kwamba ‘nimeamua kujiua mimi mwenyewe asishikiliwe mtu yoyote nimeamua kwa moyo wangu, nimeamua kumfuata Mama yangu aliyetangulia mbele za haki miaka mingi iliyopita”.amesema
Mazishi ya marehemu Ally Hamis yamefanyika leo jioni mahali alipozaliwa katika kijiji cha Itwangi Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ambapo Mwenyekiti Bwana Kisendi Lubinza ametumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi wa kijiji cha Itwangi kuacha tabia hizo za kuchukua maamuzi magumu na badala yake wanapaswa kufikisha changamoto kwenye uongozi wa kijiji ili kuona namna bora ya kutatua.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi amethibitisha juu ya tukio hilo kuwa Ally Hamis amefariki Dunia kwa kujinyonga chumbani kwake katika kijiji cha Itwangi Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
“Ni kweli mtu huyo alijinyonga na akaacha ujumbe kuwa anamadeni kwahiyo askari wameshaenda wakakagua eneo la tukio walikuwa na daktari mwili umefanyiwa uchunguzi na walikabidhiwa ndugu”amesema ACP Magomi
Post a Comment