" WAKIMBIA UFADHILI,WENZAO WAKINUFAIKA NA ELIMU,VITENDEA KAZI!

WAKIMBIA UFADHILI,WENZAO WAKINUFAIKA NA ELIMU,VITENDEA KAZI!

Na Ibrahim Rojala, Misalaba Media

Licha ya serikali kwa ushirikiano na wadau mbalimbali wa maendeleo kutekeleza miradi mbalimbali yenye lengo la kumkwamua mtoto wa kike dhidi ya madhara ya mimba na ndoa za utotoni,ukeketaji pamoja na ukatili wa kijinsia bado kuna changamoto ya kukosa utayari miongoni mwa walengwa wa miradi hiyo.

Hayo yamebainishwa na Bi.Joyce Kessy ambaye ni Mratibu wa Mradi wa Chaguo langu Haki yangu unaotekelezwa na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WILDAF)kwa ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu(UNFPA)kwa ufadhili wa serikali ya Finland amesema kwamba licha ya  kuwezesha wasichana 290 kujiunga na elimu ya ufundi Stadi,wanafunzi 263 kati yao ndio waliofanikiwa kuhitimu.

“Unajua wengi tunaowachukua wana umri mdogo,wako nje ya shule akili za ujana mwingi na utoto zinawasumbua,mwingine aliiacha tu kwasababu hataki kuendelea,binti mpaka analia!Lakini wengine wakati tunawachukua walikuwa wajawazito,changamoto za ujauzito ziliwafanya washindwe kuendelea na tulikutana na waliokuwa wanatoroka vyuoni  na kwenda kwa kiboyfriend kwa kisingizio cha kwenda nyumbani”

Aidha Bi. Joyce ameeleza kwamba kupitia mradi huo wamefanya kazi mbalimbali kwa kushirikiana na viongozi wa serikali,dini.kimila na wadau wengine wa mendeleo ili kuhakikisha wanakusanya nguvu ya pamoja ili kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia,ndoa za utotoni pamoja na ukeketaji.

“Tumewezesha mabinti kupata elimu ya kujitambua,kutambua fursa za kiuchhumi zinazowazunguka ili kuweza kujikwamua kiuchumi pamoja na kupata nguvu ya kujitegemea na kufanya maamuzi,kwa ujumla tumewawezesha kupata elimu ya stadi za maisha na elimu ya Mafunzo ya Ufundi Stadi kutoka VETA”amesema Joyce Kessy.

Wakizungumza kuhusiana na uwepo wa changamoto hii, Prisca Magai,Juliana Eliasi na Sai Mathias ambao ni wakazi wa mkoa wa Shinyanga wameeleza sababu mbalimbali zinazosababisha uwepo wa hali hiyo wakitaja mazingira wanayotoka wanaopatiwa misaada, baadhi ya mabinti kuyazoea maisha ya awali ambayo licha ya kuonekana kuwa ni changamoto ya kimaisha wao wanaona kwamba ni sawa kuishi hivyo pamoja na kutotambua faida ya kile wanachosaidiwa kwa maisha yao ya baadae.

Wakati wengine safari yao ikiishia njiani kuna wale waliojifunga vibwebwe na kufika mwisho wa safari ya kimasomo waliyoianza kupitia mradi wa chaguo langu haki yangu na hatimaye kuhitimu na kumaliza masomo yao,Beatrice Masanja na Vanessa Joseph kutoka wilayani Kishapu wanaeleza kwamba kabla  ya kupata ufadhili wa masomo ya ufundi stadi kupitia mradi huo walikuwa wakiishi tu mitaani bila ya kuwa na tumaini lolote kabla ya kukabidhiwa vitendea kazi baada ya kuhitimu.

Mradi wa Chaguo langu Haki yangu uliobua uwepo wa changamoto hii unatekelezwa katika mikoa ya Shiyanga na Mara katika wilaya za Kishapu,Kahama,Mara na Tarime  ukilenga kutokomeza vitendo vya Ukatili wa Kijinsia,Ndoa za Utotoni na Ukeketaji kwa mabinti walio nje ya mfumo wa elimu wenye umri wa miaka kati ya 15-24 mpaka sasa umeweza kuwafikia mabinti 1,081 kupitia progamu mbili ambazo ni elimu ya stadi za maisha na elimu ya ufundi stadi zinazoendeshwa ndani ya mradi husika.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post