Rushwa ni tatizo la kidunia lenye madhara makubwa kwa mtu, jamii, nchi na
mataifa kwa ujumla. Rushwa imetumika kupoka haki za watu kwa kumnyang’anya haki
yeye aliyeistahili na kumpa yule asiyeistahili kwa sababu mwenye jukumu la
kutoa haki amepokea hongo au kaahidiwa kupewa hongo ili apindishe sheria.
Ni kwa sababu ya rushwa wapo vijana wanaokosa
fursa za masomo au za kupata mikopo ya kibiashara na wengine kupendelewa na
kupewa fursa hizo japo hawana sifa kwa kuwa wametoa rushwa.
Rushwa
imewanyima wananchi wengi hasa maskini fursa ya kupata huduma bora za kijamii
kama vile majisafi na salama, elimu bora, afya, makazi au miundombinu bora ya
barabara kwa fedha inayotengwa kuboresha huduma hizi kuhujumiwa na watendaji au
watu wachache na kuitumia kwa maslahi binafsi.
Tumeshuhudia pia matukio ambayo vitendo vya
rushwa vimetumika kuchepusha au kuvujisha mapato ya Serikali hivyo kuikosesha
Serikali fedha ya kutoa au kuboresha huduma kwa umma.
Mapambano dhidi
ya rushwa yametamkwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka
1977 katika Ibara ya 9(h) ambapo Serikali na taasisi zake zimetakiwa
kuhakikisha aina zote za dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa, uonevu au
upendeleo zinaondolewa nchini. Ikiwa ni miaka mitatu sasa tangu Machi 19, 2021 siku
ambayo Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliapa kuwa Rais wa sita wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na kuahidi kuilinda, kuhifadhi na kuitetea Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yapo mengi ya kujivunia yaliyofanyika katika
mapambano dhidi ya rushwa nchini katika kipindi hicho.
Alipohutubia Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania mnamo Aprili 22, 2021 jijini Dodoma, Rais Samia alieleza dhamira ya
dhati ya Serikali ya kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa kwa kutowaonea aibu
viongozi na watumishi wazembe, wezi na wabadhirifu wa mali za umma. “Tutaendeleza
pia juhudi za kupambana na rushwa kwenye utumishi wa umma,” alisisitiza
Rais Dkt Samia. Dhamira hii inadhihirika kwa matokeo yanayotokana na hatua
zilizochukuliwa kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa nchini.
Mathalani, taarifa ya utafiti uliofanywa na Transparency International ya mwaka 2023 kuhusu Corruption Perception Index (CPI) inaonesha kuwa Tanzania imefanya
vizuri na kupata alama 40 na kushika nafasi ya 87 kati ya nchi 180
zilizofanyiwa utafiti, ikilinganishwa na alama 38 ilizopata mwaka 2022
ambapo ilishika nafasi ya 94. Tanzania, kwa mujibu wa taarifa hiyo,
imeshika nafasi ya pili katika mapambano dhidi ya rushwa katika ukanda wa
Afrika Mashariki ikitanguliwa na nchi ya Rwanda.
Aidha, ili kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa hivyo
kuhakikisha ustawi wa umma, Serikali imefanya maboresho ya Sheria ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa, Sura 329 ili iendane na mazingira ya sasa ya kiuchumi,
kijamii na kiteknolojia. Muswada wa maboresho hayo ya Sheria upo katika hatua
ya kuwasilishwa Bungeni. Hii ni hatua muhimu katika mapambano haya.
Pia, Serikali imeimarisha uwezo wa kiutendaji
wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kuiwezesha kwa
rasilimali watu, rasilimali fedha, vitendea kazi pamoja na mafunzo ya weledi
kwa watumishi. Mapema
mwaka huu 2024, Serikali imetoa kibali cha ajira za watumishi 350 hivyo
kufanya idadi ya watumishi wapya wa TAKUKURU katika kipindi cha miaka mitatu ya
uongozi wa Rais Samia kufikia 880. Uimarishaji huu wa TAKUKURU umeifanya
kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi hivyo kuimarisha mapambano dhidi ya
rushwa nchini.
Kutokana na uwezeshaji wa TAKUKURU uliofanywa
na Serikali, kiasi cha Shilingi bilioni
201.72 imedhibitiwa na kurejeshwa Serikalini kupitia operesheni
mbalimbali za uchunguzi wa tuhuma za rushwa pamoja na ufuatiliaji
wa miradi ya maendeleo. Sehemu ya fedha hii imetumika kutekeleza miradi mingine ya maendeleo kama
vile ujenzi wa vituo vya afya, manunuzi ya dawa na vifaa tiba pamoja na ujenzi wa shule na
barabara ili kuleta ustawi wa wananchi na maendeleo endelevu ya Taifa.
Serikali pia imetaifisha mali zenye thamani
ya Shilingi bilioni 2.14 zikijumuisha
nyumba, viwanja na magari. Aidha, miradi ya maendeleo 3,576 yenye thamani
ya Shilingi trilioni 16.76 ilifuatiliwa kwa madhumuni ya kuhakikisha kuwa fedha hiyo inatumika kadiri ilivyokusudiwa ili kuwaletea wananchi maendeleo.
Vilevile, katika kipindi hiki cha miaka mitatu, uchunguzi wa tuhuma za vitendo vya rushwa uliendelea
na pale penye ushahidi na kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kesi
zilifunguliwa na kuendeshwa mahakamani. Jumla ya kesi 1,922 za rushwa ziliendeshwa mahakamani
zikiwamo kesi 19 zilizofunguliwa
katika Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ya Mahakama Kuu ya
Tanzania. Mahakama ilitoa maamuzi katika kesi 1,303 za rushwa ambapo katika kesi 801 sawa na asilimia 61 Jamhuri ilishinda baada ya washtakiwa
kupatikana na hatia ya kutenda makosa ya rushwa na kuhukumiwa kifungo jela au
kulipa faini.
Serikali inayoongozwa
na Rais Samia pia imeimarisha mapambano dhidi ya rushwa kwa kuipatia TAKUKURU
fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya ofisi. Fedha hiyo imewezesha kuanzisha na kukamilisha ujenzi wa majengo ya ofisi za
TAKUKURU za mikoa ya Kilimanjaro na Simiyu na kukamilisha ujenzi wa majengo ya
ofisi za wilaya saba za Kilolo mkoani Iringa, Kongwa (Dodoma), Kiteto
(Manyara), Mvomero (Mvomero), Liwale (Lindi), Nyasa (Ruvuma) na Momba (Songwe).
Vilevile, ujenzi wa jengo la Makao Makuu jijini Dodoma, majengo mawili ya mikoa ya Iringa na Shinyanga pamoja na
majengo matano ya ofisi za wilaya za Nkasi (Rukwa), Nzega (Tabora), Kishapu
(Shinyanga), Monduli (Arusha) na Rombo mkoani Klimanjaro unaendelea.
Serikali pia imeiwezesha TAKUKURU kwa
fedha ya kuendelea kutekeleza jukumu lake la kuelimisha umma kuhusu madhara ya
rushwa na kuuhamasisha ushiriki katika mapambano dhidi ya adui rushwa. Hii ni sehemu ya jitihada za
kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa ambapo baadhi ya wadau wamehamasika na kuchangia kuzuia vitendo vya rushwa kwa kuacha
kushiriki vitendo hivyo au kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa huku wengine
wakipata ujasiri na kujitokeza kutoa ushahidi katika kesi za rushwa mahakamani.
Uelimishaji umma umefanyika kwa
makundi mbalimbali katika jamii kuanzia vijijini hadi mijini kupitia mikutano,
minada, magulio, midahalo, semina, warsha, mbio za Mwenge wa Uhuru, vipindi vya
redio, vipindi vya televisheni, na machapisho mbalimbali. Pia, elimu kwa umma
imetolewa kupitia maonesho ya kitaifa na kimataifa yanayofanyika kila mwaka
nchini kama vile maonesho ya Wakulima (Nanenane) na Maonesho ya Kimataifa ya
Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Ili
kuongeza ushiriki wa wadau katika kuzuia vitendo vya rushwa, Programu ya
TAKUKURU - Rafiki ilizinduliwa 20 Disemba, 2022. Programu hii imelenga
kushirikisha wadau kutatua kero katika utoaji wa huduma kwa umma na utekelezaji
wa miradi ya maendeleo ambazo zikiachwa bila kutatuliwa zinaweza
kusababisha kutokea kwa vitendo vya rushwa. Utekelezaji wa Programu hii umekuwa
wenye mafanikio ambapo kero nyingi zilizoibuliwa
zimetatuliwa hivyo kuzuia vitendo vya rushwa na kuboresha huduma zinazotolewa
kwa umma.
Katika hatua nyingine, mwaka 2023, Tanzania ilikuwa mwenyeji wa Maadhimisho ya
Siku ya Mapambano Dhidi ya Rushwa Barani Afrika yaliyofanyika jijini Arusha
kuanzia Julai 9-11, 2023. Hii ilikuwa heshima kubwa kwa Taifa na inayoashiria
imani ya Mataifa mengine ya Afrika pamoja na Umoja wa
Afrika kwa Tanzania katika suala la mapambano dhidi ya rushwa. Wadau mbalimbali
wa mapambano haya kutoka ndani na nje ya Tanzania wakiwemo kutoka sekta ya
umma, sekta binafsi na asasi za kiraia walishiriki maadhimisho hayo.
Akihutubia wadau
hao siku ya kilele Julai 11, 2023, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Dkt. Samia pamoja na mambo mengine aliwatahadharisha watu wanaojihusisha
na rushwa kuhusu mienendo yao. “Walarushwa
wanapaswa kufahamu kuwa nchi zetu si vichaka vya kuficha fedha zilizotokana na
rushwa au kufuga walarushwa. Tunataka dunia nzima ifahamu kuwa, Afrika si
salama kwa walarushwa na hilo lionekane kwa vitendo kupitia hatua
tunazozichukua dhidi ya walarushwa”, alisisitiza Rais Samia.
Mheshimiwa Rais
Samia hakuishia kutoa onyo hilo bali aliueleza ulimwengu mafanikio ya hatua
zilizochukuliwa na Tanzania kuidhibiti rushwa, yaani kazi zilizofanyika kuzuia
na kupambana na rushwa. Mathalani, alisema kuwa katika kipindi cha miaka
mitatu, kupitia mapambano dhidi ya rushwa Serikali iliokoa zaidi ya Shilingi bilioni 139 ya fedha ya umma.
“Fedha hizo ukinipa mimi sasa hivi
nikifumba macho nakwambia nazipeleka kununua vifaa tiba,” alisema Mhe. Dkt.
Samia.
Rais Samia
aliwaomba viongozi barani Afrika kushirikiana katika kupambana na vitendo vya
rushwa na kusisitiza kuwa moja ya vikwazo vikubwa vya maendeleo barani Afrika
ni janga la rushwa ambalo linadhoofisha mifumo ya kitaasisi na kuathiri mipango
na mikakati ya kujikomboa kiuchumi. Pia, alitumia jukwaa la maadhimisho hayo,
pamoja na mambo mengine, kumtaka kila Mtanzania kujitathmini ni kwa namna gani
anadhibiti rushwa huku akiirejea kaulimbiu ya TAKUKURU. ‘‘Kuzuia Rushwa ni Jukumu Lako na Langu ; Tutimize
Wajibu Wetu. Ni kaulimbiu nzito na kaulimbiu inayotupa mtihani hasa sisi
Watanzania, tujitizame sisi wenyewe mmojammoja, tunaendana na kaulimbiu hii ?’’
alihoji Rais Samia.
”Nitasimama imara kwenye mapambano dhidi ya rushwa”
hii ni ahadi aliyoitoa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania wakati anapokea taarifa ya utendaji kazi wa TAKUKURU Machi
28, 2021 katika Ikulu ya Chamwino ikiwa ni siku tisa tangu ale kiapo cha kuwa
Rais. Tunawiwa kusema, ahadi hii ameitekeleza kwa vitendo na Watanzania hatuna
budi kusimama imara na kuungana naye kwenye mapambano haya kwa kuizingatia
kaulimbiu ”Kuzuia Rushwa ni Jukumu Lako
na Langu; Tutimize Wajibu Wetu.”
Post a Comment