" MAADHIMISHO YA MIAKA 71: JUMUIYA YA WAZAZI CCM WILAYA YA SHINYANGA MJINI YASISITIZA MALEZI BORA NA ULINZI WA AMANI

MAADHIMISHO YA MIAKA 71: JUMUIYA YA WAZAZI CCM WILAYA YA SHINYANGA MJINI YASISITIZA MALEZI BORA NA ULINZI WA AMANI


Na Mapuli Kitina Misalaba

Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini imeadhimisha miaka 71 tangu kuanzishwa kwa jumuiya hiyo, huku viongozi wakitoa wito wa kuendelea kulinda maadili ya jamii, kuimarisha malezi ya watoto na kudumisha amani ya Taifa.

Maadhimisho hayo yamefanyika katika Kijiji cha Galamba, Kata ya Kolandoto katika Manispaa ya Shinyanga, ambapo mgeni rasmi ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhe. Anord Makombe.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mhe. Makombe amesema Jumuiya ya Wazazi ina nafasi kubwa katika jamii kutokana na jukumu lake la kusimamia malezi na maadili ya vijana, hasa katika kipindi hiki ambacho kumekuwa na changamoto ya mmomonyoko wa maadili.

Amesema jamii inapaswa kushirikiana kwa pamoja na taasisi mbalimbali kuhakikisha watoto wa kiume na wa kike wanapatiwa ulinzi na mazingira bora yatakayowasaidia kutimiza ndoto zao kupitia elimu na maadili mema.

“Jumuiya ya wazazi leo inaadhimisha miaka 71 kiwilaya na maadhimisho haya yanafanyika hapa Galamba. Jumuiya hii ina majukumu mengi ikiwemo kushughulikia malezi ya vijana. Leo tunashuhudia mmomonyoko wa maadili katika jamii, hivyo tunatakiwa kushirikiana kuhakikisha watoto wetu wanapata malezi bora, elimu na kutimiza ndoto zao,” amesema Makombe.

Aidha, Magombe amewataka wananchi kuendelea kudumisha umoja, mshikamano na upendo huku wakimuomba Mungu katika maisha yao ya kila siku, akieleza kuwa hali hiyo itasaidia kupunguza vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinavyoendelea kujitokeza katika baadhi ya maeneo.

“Tuendelee kuwa wamoja na kushikamana ili watu waendelee kuishi katika amani na upendo. Watu wakimuogopa Mungu itakuwa vigumu kufanya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto. Leo tunaona hata baadhi ya wazazi wanawafanyia watoto wao ukatili, hivyo jamii inapaswa kusimama pamoja kupinga hali hiyo,” ameongeza.

Katika hatua nyingine, Mhe. Makombe amesisitiza umuhimu wa kulinda amani ya Tanzania, akiwataka wananchi kuwa wazalendo na kutoa taarifa mapema pale wanapoona viashiria vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa nchi.

Amesema amani iliyopo nchini ni urithi mkubwa ulioasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Julius Nyerere na kuendelezwa na viongozi waliomfuatia, hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kuilinda.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mzee Fue Mrindoko, amesisitiza umuhimu wa umoja na mshikamano miongoni mwa wanajumuiya pamoja na wananchi kwa ujumla ili kuendelea kujenga jamii yenye maadili na ustawi.

Naye Katibu wa Jumuiya hiyo wilayani humo, Bi. Doris Kibabi, amesema katika kuadhimisha miaka 71 ya jumuiya hiyo wamefanikiwa kutekeleza shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kutoa misaada kwa watu wenye uhitaji pamoja na wagonjwa waliolazwa hospitalini.

Amesema pia jumuiya hiyo imepanda miti zaidi ya 361 ikiwa ni sehemu ya kampeni ya utunzaji wa mazingira na kuhamasisha wananchi kushiriki katika uhifadhi wa mazingira kwa kupanda miti katika maeneo mbalimbali.

Katika maadhimisho hayo, Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini imetoa vyeti vya pongezi kwa taasisi na idara mbalimbali zilizofanya vizuri katika utoaji wa huduma kwa jamii.

Miongoni mwa waliotunukiwa vyeti hivyo ni Idara ya Mazingira ya Manispaa ya Shinyanga kwa kuendelea kuwa kinara wa usafi kitaifa, Idara ya Elimu, Idara ya Ustawi wa Jamii pamoja na Jumuiya ya kupinga ukatili ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) kwa mchango wao katika kupambana na vitendo vya ukatili katika jamii.

Katibu wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Hamisa Chacha akizungumza.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini Mzee Fue Mrindoko akisisitiza umuhimu wa umoja na mshikamano kwa wanajumuiya pamoja na wananchi wakati wa maadhimisho ya miaka 71 ya jumuiya hiyo.

Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini Bi. Doris Kibabi akieleza shughuli zilizotekelezwa na jumuiya hiyo ikiwemo utoaji wa misaada na upandaji wa miti zaidi ya 361 kwa ajili ya utunzaji wa mazingira.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini Mhe. Anord Makombe akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 71 ya Jumuiya ya Wazazi ya CCM yaliyofanyika katika Kijiji cha Galamba, Kata ya Kolandoto Manispaa ya Shinyanga.


MR. BLACK



Picha yao ya pamoja. Katibu na Mwenyekiti.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhe. Anord Makombe akiongoza zoezi la upandaji miti katika Kijiji cha Galamba, Kata ya Kolandoto ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 71 ya Jumuiya ya Wazazi ya CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini.
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Bi. Doris Kibabi akishiriki zoezi la upandaji miti katika Kijiji cha Galamba, Kata ya Kolandoto ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 71 ya Jumuiya ya Wazazi.


Mjumbe wa kamati ya utekelezaji ya Jumuiya ya wazazi Bi. Husna Maige akipanda mti.

Post a Comment

Previous Post Next Post