" MSANGANI WAWAKATAA WAPINZANI HADHARANI, WAAHIDI KUMPA USHINDI MGOMBEA UDIWANI CCM

MSANGANI WAWAKATAA WAPINZANI HADHARANI, WAAHIDI KUMPA USHINDI MGOMBEA UDIWANI CCM



Na Dismas Lyassa, Kibaha

WANANCHI wa mitaa mbalimbali ya Kata ya Msangani, Halmashauri ya Mji Kibaha mkoani Pwani ambako leo Machi 20 uchaguzi mdogo wa udiwani unafanyika wameonekana hadharani wakiwakataa wagombea wa vyama vya upinzani na kuahidi kumpigia kura mgombea wa CCM ndugu Gunze Yohana Chongela (aliyeshika mkono kifua) wakidai kuwa vyama vya upinzani katika kata yao havina hata ofisi na vinaonekana tu wakati wa uchaguzi.

“Inatia aibu sana, vyama vya upinzani vyote vilivyosimamisha wagombea havina hata ofisi, tukisema tuwape udiwani huyo diwani anapokosea katika utendaji wake atashughulikiwa na chama chake kivipi wakati hata ofisi hazina,” alisema mwananchi mmoja wa Msangani aliyejitambulisha kwa jina la Mwanahamisi Haule maarufu kwa jina la Mama Deborah.



Mwananchi mwingine akaongeza kuwa anachofahamu chama imara huzaa Serikali imara. Kwamba, uimara wa CCM sio wa kutiliwa shaka, hivyo wanaona ni sahihi kuchagua mgombea wa CCM ili aweze kuwapigania maendeleo katika kata yao.

“Mama Samia, Rais wetu kipenzi ametufanyia mambo mengi sana katika eneo letu ikiwamo kutujengea Zahanati, tunataka kumpa kura za kutosha mgombea wa CCM ili aweze kuingia kwenye vikao mbalimbali vya chama na Serikali kutusaidia kuharakisha maendeleo katika eneo letu,” anasema.

Utafiti unaonyesha kuwa katika mitaa yote iliyoko katika Kata ya Msangani wananchi hawako tayari kuwapigia kura wagombea wa upinzani, mojawapo ya sababu ni udhaifu wa vyama hivyo, lakini zaidi vyama hivyo vya upinzani kukosa sera thabiti za maendeleo.



“Mfano madiwani wote katika Halmashauri ya Mji Kibaha Mjini ni wa CCM, ni kweli tukiingiza mpinzani nani atamsikiliza kwenye vikao vyao vya maendeleo wilaya na kata? Ndio maana tunasema sisi chaguo letu ni mgombea Gunze, sio tu kwa sababu ni mwana CCM bali tumekuwa tukishirikiana nae katika jitihada mbalimbali za maendeleo. Hao wapinzani binafsi sijawahi kumuona hata mmoja wao katika ujenzi wa zahanati wala hata kushiriki mikutano ya maendeleo.

Post a Comment

Previous Post Next Post