Ticker

6/recent/ticker-posts

KIJANA MMOJA AUAWA KATA YA NGOKOLO, JESHI LA POLISI MKOA WA SHINYANGA LAONYA WATU KUJICHUKULIA SHERIA MKONONI

Kijana mmoja anayekadiriwa kuwa na umri wa Miaka 22 ambaye hakufahamika mara moja jina wala makazi yake amekutwa akiwa ameuawa na mwili wake kuchomwa moto na watu wasiojulikana katika mtaa wa  Mwadui Manispaa ya Shinyanga.

Misalaba Media imefika katika eneo la tukio na kuzungumza na Mwenyekiti wa mtaa huo Mwalimu Nuru Juma ambaye amekiri kuuawa kwa kijana huyo ambaye amechomwa moto mwili mzima, leo Jumatatu Juni 10,2024.

Mwenyekiti huyo ameeleza zaidi kuwa mpaka sasa haijafahamika chanzo cha mauaji  ya kijana huyo na kwamba jeshi la polisi limefika katika eneo la tukio na tayari wamechukua mwili wa marehemu huyo .

 “Leo tarehe kumi (10) muda wa saa nne nilipata taarifa kwamba kuna mtu amekufa kwenye vichaka kachomwa moto baada ya kupata taarifa hii linikwenda kuangalia nimefika pale nikakuta kweli kijana mwenye umri kama 22 hivi amechomwa moto mwili mzima na nguo hana huko uchi”.

"Baada ya kuangalia vile ilibidi nichukue hatua ya kuita Polisi waje kwenye tukio na polisi walikuja wakamchunguza na badae wakaubeba mwili, hakuna hata mtu mmoja ambaye anamfahamu kwahiyo ni kijana ambaye hajulikani ni wawapi”.amesema Mwenyekiti Mwalimu Nuru

Hili  linakuwa ni tukio la pili  na kufanya idadi ya watu waliouawa na kuchomwa moto   kufikia  watatu katika kipindi cha siku nne katika manispaa ya Shinyanga ambapo  Ijumaa Mwezi huu une  saba  watu wawili wanaosadikiwa kufanya tukio  la ujambazi waliuwawa kwa nyakati tofauti katika   kijiji cha Iwelyangula na mwingine katika kijiji cha Bugayambelele manispaa ya Shinyanga.

Misalaba Media pia imezungumza na Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi (SACP) Janeth Magomi ambaye ameelezea tukio hilo huku akiwataka wananchi kuacha tabia za kujichukulia sheria mkononi kwani ni kosa kisehria.

 “Jeshi la Polisi majira ya saa nne asubuhi tulipata taarifa kwamba maeneo ya viwanja vya Mwadui kata ya Ngokolo ndani ya Manispaa na Mkoa wa Shinyinga mtu mmoja mwanaume asiyefahamika majina wala makazi anayekadiriwa kuwa na umri kati ya Miaka 28 hadi 30 alikutwa akiwa ameuawa, askari walifika kwenye eneo la tukio na kuweza kuuchukua huo mwili”.

“Nipende kutoa rai kwa wananchi kwamba jeshi la Polisi hatutakubaliana na hiki kinachotaka kuendelea na nimeshasema mara kadha wa kadha habari ya kujichukulia sheria mkononi sisi hatutanyamaza na tuko chini kwa chini tunaendelea kupata taarifa fiche waliohusika na vitendo hivi ambao wanajichukulia sheria mkononi eti wao wanahasira, hakuna mtu ambaye yuko juu ya sheria na ndiyo maana vimewekwa vyombo vya kutoa haki Mahakama zipo, mahakama kuu ipo mahakama ya rufaani ipo mahakama za mwanzo lakini pia mahakama za Wilaya naza Mikoa zipo kwahiyo wananchi wasijichukulie sheria mkononi”.amesema SACP Magomi

Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi (SACP) Janeth Magomi akizungumza.

Mwenyekiti wa mtaa huo Mwalimu Nuru Juma akizungumza na Misalaba Media leo Jumatatu Juni 10,2024.


 

Post a Comment

0 Comments