Katibu wa siasa, itikadi na uenezi wa CCM Wilaya ya Shinyanga mjini Said Bwanga akisoma taarifa hiyo leo Ijumaa Machi 13, 2026.Na Mapuli Kitina Misalaba
Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya
Shinyanga mjini imewasilisha mapendekezo yake kufuatia kupokea na kujadili
taarifa ya Serikali kuhusu utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya
mwaka 2025–2030 kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2025, kwa mujibu wa Ibara ya
75 (3) na Ibara ya 76 (4) ya Katiba ya CCM Toleo la Mei 2025.
Taarifa hiyo imesomwa na katibu wa siasa, itikadi na
uenezi wa CCM Wilaya ya Shinyanga mjini Said Bwanga na kwamba kikao hicho kimepokea,
kujadili na kutoa ushauri, maelekezo pamoja na maagizo kuhusu utekelezaji wa
Ilani ya Chama, sambamba na kusimamia utekelezaji wa siasa na maelekezo ya
chama kwa ujumla.
Katika hatua hiyo, Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu
ya CCM Wilaya baada ya kupokea taarifa ya Serikali iliyowasilishwa na Ofisi ya
Mkuu wa Wilaya, iliijadili kwa kina na kisha kutoa mapendekezo mbalimbali kwa
kuzingatia utekelezaji wa miradi na maendeleo ya sekta mbalimbali.
Kwa mujibu wa tathmini ya Kamati ya Siasa, imebainika
kuwa miradi mingi iliyotekelezwa katika kipindi hicho imefanikiwa kutokana na
fedha zilizotolewa na Serikali Kuu kupitia Hazina, michango ya wafadhili pamoja
na nguvu za wananchi.
Taarifa hiyo pia imeonyesha kuwa bajeti ya Halmashauri
katika utekelezaji wa maendeleo kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ilikuwa jumla ya
shilingi 42,285,083,200. Kati ya fedha hizo, mapato ya ndani yalikuwa shilingi
7,463,922,000, ruzuku ya uendeshaji wa ofisi shilingi 2,007,013,000, miradi ya
maendeleo kupitia ruzuku ya Serikali Kuu na wahisani shilingi 9,215,299,000,
huku ruzuku ya mishahara ikiwa shilingi 23,597,949,200.
Hadi kufikia Desemba 2025, jumla ya shilingi
17,877,245,861.78 zilikuwa zimetumika, sawa na asilimia 92 ya mapato yote
yaliyokusudiwa kutumika katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.
Baada ya kufanya ukaguzi wa miradi mbalimbali, Kamati
ya Siasa imebaini kuwa miradi mingi iliyotekelezwa imefikia hatua nzuri huku
michache iliyobaki ikiwa katika hatua za mwisho za utekelezaji. Kutokana na
hali hiyo, Kamati imehimiza juhudi zaidi ziwekwe ili kukamilisha miradi yote
iliyopangwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha.
Hivyo, Kamati ya Siasa ya Wilaya imependekeza kuwa
Halmashauri isianzishe miradi mipya wakati bado kuna miradi ambayo
haijakamilika, pamoja na Serikali kuongeza nguvu katika ukusanyaji wa mapato ya
ndani ili kuongeza uwezo wa kutekeleza miradi ya maendeleo.
Katika sekta ya Kilimo na Mifugo, Kamati imependekeza
Serikali iendelee kutoa elimu kwa wakulima na wafugaji kuhusu mbinu bora za
kilimo na ufugaji wa kisasa ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na
biashara.
Aidha, katika eneo la mifugo na uvuvi, Serikali imeshauriwa
kuwahimiza na kuwaelekeza Maafisa Ugani wa Kata kufanya kazi kwa karibu na
wananchi katika kuwasaidia kupata kinga na mbinu bora za kudhibiti magonjwa ya
mifugo. Serikali pia inashauriwa kuendelea kuunda vikundi vya SACCOs kwa
wafugaji na kuvipa kipaumbele katika shughuli za kununua na kuuza mifugo kwa
wanunuzi au viwanda ili kulinda bei ya soko la ng’ombe, mbuzi na kondoo.
Kwa upande wa sekta ya miundombinu, Kamati
imependekeza Serikali ya Wilaya kuchukua hatua za kuhamasisha wananchi wengi
zaidi kupata hati miliki za viwanja vyao, kwani utekelezaji wa utoaji wa hati
kwa sasa haujafikia kiwango kinachoridhisha. Pia imependekezwa kupunguza
urasimu katika utoaji wa huduma hizo ili kuondoa malalamiko ya wananchi.
Vilevile Serikali imeshauriwa kuendelea kupima viwanja
na kuwapatia waombaji bila urasimu, pamoja na kulipa fidia kwa viwanja
vinavyodaiwa ili kumaliza migogoro ya ardhi katika Manispaa. Serikali pia
inapaswa kuhakikisha wananchi wanapewa viwanja vyenye namba sahihi, badala ya
kuonyeshwa viwanja kisha kuambiwa namba zitatafutwa baadaye.
Katika zoezi la ugawaji wa viwanja, Kamati imependekeza
Serikali kuweka kipaumbele kwa wananchi wanaodai viwanja, pamoja na
kuwashirikisha wananchi katika kupata gharama za upimaji wa viwanja katika
maeneo wanayoishi ili kurahisisha mchakato huo.
Kwa upande wa uwezeshaji wa wananchi kiuchumi kupitia
sekta ya maendeleo ya jamii, Kamati imependekeza Serikali kuongeza kasi ya
kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa Afya ya Jamii wa Bima za Afya. Pia
imeelekezwa kuhakikisha huduma za dawa kwa wazee katika Hospitali ya Wilaya
zinatolewa bila usumbufu.
Kamati pia imeeleza kuwepo kwa changamoto ya matumizi
ya kauli zisizo na staha kwa baadhi ya wananchi wanaoomba mikopo ya vikundi,
hali inayokatisha tamaa wanavikundi. Hivyo, Serikali inapaswa kuweka usimamizi
wa karibu kwa vikundi vilivyoundwa, kufuatilia urejeshaji wa mikopo na kutoa
ushauri ili kuhakikisha mikopo hiyo inarejeshwa ipasavyo.
Serikali Kuu pia imeshauriwa kufuatilia na
kujiridhisha kuhusu uhalali na usahihi wa vikundi vilivyopata mikopo katika
mwaka wa fedha 2025/2026.
Katika sekta ya fedha na biashara, hususan Soko Kuu la
Shinyanga, Kamati imeipongeza Serikali kwa juhudi za kuongeza vyanzo vya mapato
na kuweka kodi zinazoendana na hali ya soko la sasa. Hata hivyo, imependekeza
hatua zaidi zichukuliwe ili kuongeza mapato ya ndani na kuimarisha mfumo wa
ukusanyaji mapato.
Pia Serikali imeshauriwa kuendelea kutoa mafunzo kwa
wajasiriamali na wafanyabiashara kuhusu namna bora ya kuandaa na kufungasha
bidhaa za nafaka. Aidha, Kamati imebaini kuwa kibanda cha mfano kilichojengwa
katika soko kuu hakikidhi mahitaji ya wafanyabiashara kutokana na gharama kubwa
za ujenzi na muundo wake kutokidhi matumizi yaliyokusudiwa, hali iliyosababisha
wafanyabiashara kukikataa.
Katika sekta ya huduma za jamii, Kamati imeelekeza
Serikali kusimamia kwa karibu changamoto zinazojitokeza katika shule za msingi,
ikiwemo ujenzi wa vyoo na madarasa. Serikali pia imepongezwa kwa kujenga
miundombinu ya shule za msingi Bugayambebele, Mwenge, Kizumbi na Mwanase
iliyopo Kolandoto.
Kwa upande wa shule za sekondari, Serikali imeelekezwa
kutoa taarifa bayana kuhusu hali ya ufaulu wa wanafunzi waliojiunga na
sekondari ili kubaini kama kuna ongezeko la ufaulu au la, jambo litakalosaidia
kupima mafanikio yaliyofikiwa.
Vilevile Serikali inatakiwa kushughulikia upatikanaji
wa walimu wa masomo ya sayansi ili kuondoa upungufu uliopo. Aidha, Serikali ya
Wilaya inapaswa kusimamia kwa karibu ujenzi wa madarasa unaoendelea ili
kujiridhisha na gharama halisi za ujenzi pamoja na kuchunguza gharama za ujenzi
wa madarasa na ofisi za walimu.
Katika sekta ya afya, Serikali imeelekezwa kufuatilia
ujenzi wa Zahanati ya Mwanibu. Pia Serikali ya Wilaya imeshauriwa kushughulikia
malalamiko ya wananchi kuhusu matumizi ya kauli zisizo na staha kutoka kwa
baadhi ya wahudumu wa Hospitali ya Wilaya.
Kwa upande wa idara ya maji, Kamati imebainisha kuwa
mradi wa huduma ya maji Kolandoto unaendelea vizuri, lakini imeishauri Serikali
kuongeza kasi ili mradi huo ukamilike kwa wakati. Serikali pia imeshauriwa
kusimamia kwa karibu usambazaji wa huduma ya maji, hususan katika maeneo ya
vijijini.
Katika sekta ya ujenzi wa barabara, Kamati ya Siasa
imeeleza kutoridhishwa na maendeleo ya mradi wa ujenzi wa barabara ya lami
kutoka Nguzo Nane hadi Mwawaza, kwani mradi huo umechelewa kukamilika na
kuwasababishia wananchi usumbufu. Hivyo Serikali imeelekezwa kusimamia kwa
karibu utekelezaji wa mradi huo.
Vilevile Kamati haijaridhishwa na maendeleo ya ujenzi
wa stand ya Mkoa wa Shinyanga, ambapo imeelezwa kuwa mradi huo uko nje ya muda
uliopangwa na kuna malalamiko ya vibarua kutolipwa kwa wakati pamoja na
kutokuzingatiwa kwa baadhi ya taratibu za utekelezaji wa miradi mikubwa.
Kutokana na hali hiyo, Kamati imeielekeza Serikali kusimamia kwa karibu
utekelezaji wa mradi huo.
Kamati ya Siasa imempongeza Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuiletea
Wilaya miradi mingi ya maendeleo ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kukuza
maendeleo na kuifanya kuwa miongoni mwa wilaya zinazoendelea kwa kasi nchini.
Pia Kamati imeipongeza Serikali ya Mkoa na Wilaya kwa
usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo, na kumpongeza Mbunge wa Jimbo la
Shinyanga Mjini ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Patrobas
Katambi, kwa mchango wake katika maendeleo ya Wilaya hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro,
amesema amepokea maelekezo na mapendekezo yote yaliyotolewa na Kamati ya Siasa
ya Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya na kuahidi kuyafanyia kazi kwa kuyasimamia
ipasavyo ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi.
Amesema Serikali ya Wilaya ya Shinyanga itaongeza
nguvu katika kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ile iliyoelezwa
kuwa na changamoto, sambamba na kuhakikisha maagizo yaliyotolewa na Kamati ya
Siasa yanatekelezwa kwa wakati kwa lengo la kuharakisha maendeleo na kuboresha
huduma kwa wananchi.
Katibu wa siasa, itikadi na uenezi wa CCM Wilaya ya
Shinyanga mjini Said Bwanga akisoma taarifa hiyo leo Ijumaa Machi 13, 2026.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, akizungumza. 
Wajumbe wa kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Shinyanga mjini wakifuatilia taarifa ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho ambayo imewasilishwa leo Ijumaa Machi 13, 2026 katika ukumbi wa mikutano uliopo ofisi za CCM Mkoa wa Shinyanga.

Wajumbe wa kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Shinyanga mjini wakifuatilia taarifa ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho ambayo imewasilishwa leo Ijumaa Machi 13, 2026 katika ukumbi wa mikutano uliopo ofisi za CCM Mkoa wa Shinyanga.

Wajumbe wa kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Shinyanga mjini wakifuatilia taarifa ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho ambayo imewasilishwa leo Ijumaa Machi 13, 2026 katika ukumbi wa mikutano uliopo ofisi za CCM Mkoa wa Shinyanga.

Wajumbe wa kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Shinyanga mjini wakifuatilia taarifa ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho ambayo imewasilishwa leo Ijumaa Machi 13, 2026 katika ukumbi wa mikutano uliopo ofisi za CCM Mkoa wa Shinyanga.

Wajumbe wa kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Shinyanga mjini wakifuatilia taarifa ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho ambayo imewasilishwa leo Ijumaa Machi 13, 2026 katika ukumbi wa mikutano uliopo ofisi za CCM Mkoa wa Shinyanga.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga mjini Mhe. Anord Makombe, akiandika maoni, mapendekezo na maswali mbalimbali yanayoulizwa na wajumbe.🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254


















Post a Comment