Na Edington Mukiza Ezron, Misalaba Media
Wananchi mkoani Shinyanga wameungana na Watanzania
wengine kuadhimisha kumbukizi ya miaka mitano ya kifo cha aliyekuwa Rais wa
Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, kwa
kukumbuka na kuthamini mchango wake katika maendeleo ya taifa.
Baadhi ya wananchi katika Manispaa ya Shinyanga,
wakizungumza na Misalaba Media leo Machi 17, 2026, wamesema hayati Magufuli
ataendelea kukumbukwa kwa uadilifu wake, uchapakazi pamoja na msimamo wake
thabiti katika kusimamia rasilimali za nchi.
Mmoja wa wananchi hao, Daud Peter Philipo, amesema
kuwa kuna mambo mengi mazuri aliyoyaacha hayati Magufuli ambayo yanapaswa
kuenziwa na kizazi cha sasa na kijacho.
Ameeleza kuwa kiongozi huyo aliweka kipaumbele katika
uwajibikaji na nidhamu ya kazi, hali iliyochochea maendeleo ya uchumi na
kuongeza imani ya wananchi kwa serikali yao.
“Watanzania hatuna budi kuyaenzi mema yote
aliyoyafanya, kwani yamechangia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi na kuimarisha
ustawi wa taifa kwa ujumla,” amesema Philipo.
Kwa upande wake, mjasiriamali Steward Mathias amesema
anatamani kuona serikali ya sasa ikiendeleza yale yote mazuri yaliyoanzishwa na
hayati Magufuli, hususan katika kusikiliza kero za wananchi wa kada zote, jambo
alilodai kuwa ni msingi muhimu wa utawala bora na demokrasia.
Mathias ameongeza kuwa katika kipindi cha uongozi wa
hayati Magufuli, Tanzania ilipiga hatua kubwa katika sekta ya miundombinu,
ikiwemo ujenzi wa barabara za kisasa na madaraja ya juu (flyovers) yaliyosaidia
kupunguza msongamano wa magari mijini, sambamba na kuboreshwa kwa huduma za
kijamii kama maji, umeme na elimu.
Aidha, wananchi hao wamekumbusha umuhimu wa kuenzi
misingi ya maadili aliyokuwa akiisisitiza hayati Magufuli, ikiwemo kuwa na
imani, hofu ya Mungu na uzalendo, wakieleza kuwa hayo ni nguzo muhimu katika
kujenga jamii imara na yenye maendeleo.
Maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka mitano ya kifo cha
hayati Magufuli yamefanyika kitaifa nyumbani kwake kwa hayati Magufuli Chato
mkoani Geita, ambapo viongozi mbalimbali na wananchi wameshiriki ibada maalum
ya kumuombea pamoja na kutembelea kaburi lake, ikiwa ni ishara ya heshima na
kuthamini mchango wake kwa taifa.

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment