Na Mapuli
Kitina Misalaba
Mchungaji Charles Lugembe wa Kanisa la AICT
Kambarage amewahimiza Wakristo kujitokeza kwa wingi kwenye zoezi la
kujiandikisha wapiga kura ambalo linatarajiwa kuanza rasmi tarehe 21 Agosti
mwaka huu katika Mkoa wa Shinyanga.
Ameyasema hayo
leo wakati akisoma matangazo maalum katika ibada ya Jumapili leo Agosti 18,2024
ambapo amewakumbusha
wakristo kuwa mfano katika jamii kujitokeza kwenye zoezi hilo ili kuwa na sifa
za kuwa mpiga kura halali.
"Kuhusu daftari la mpiga kura,
taifa niwajulishe waumini kwamba tumepokea barua ya serikali inasema kuwa
tarehe 21 mpaka tarehe 27 zoezi hilo katika Manispaa yetu ya Shinyanga litakuwa
linafanyika, hasa wanaohusika ni wale ambao walishaharibu kadi zao na wale
ambao wamefika umri wa kuanza kupiga kura, miaka 18, wakapate nafasi ya
kujiandikisha wapate kadi ya mpiga kura kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu, kwahiyo
niwaombe Wakristo ambao mmefikia umri, mkajiandikishe sasa kuna wengine
wamepoteza, wengine zimeharibika, basi tuzione ofisi husika kwa ajili ya jambo
hilo."amesema
Mchungaji Lugembe
Misalaba
Media ilizungumza na baadhi ya waumini wa kanisa hilo, ambao wameahidi
kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo huku wakieleza umuhimu wa kushiriki
katika mchakato wa kujiandikisha wapiga kura kwa maendeleo ya taifa.
Waumini
hao wamesisitiza kuwa, kujiandikisha ni wajibu wa kila raia mwenye sifa, ili
kuhakikisha wanachangia katika kuleta mabadiliko ya kijamii na kiuchumi kupitia
uchaguzi.
Zoezi la
kujiandikisha wapiga kura ni muhimu, hasa kwa wale ambao wamefikia umri wa
kupiga kura kwa mara ya kwanza na wale ambao kadi zao za awali zimepotea au
kuharibika. Serikali imeweka wazi kuwa zoezi hilo Mkoani Shinyanga litafanyika
kwa muda wa siku saba pekee, kuanzia Agosti 21 hadi 27, hivyo ni muhimu kwa
wananchi kutumia muda huu kujiandikisha .
Aidha katika mahubiri yake Mchungaji mstaafu wa
Kanisa la AICT Ndala, Zabron Mang'wenhula, amewahimiza waumini wa Kanisa la
AICT Kambarage kutokata tamaa wanapopitia majaribu na changamoto katika maisha
ya Kikristo ambapo amesisitiza umuhimu wa kusaka ushauri wa kiroho na kutafuta
msaada kwa viongozi wa kiroho wakati wa
majaribu.
"Maisha
ya Ukristo yanaweza kuanguka kwenye majaribu, usikate tamaa. Tafuta ushauri,
mtafute Yesu, kaa machoni pa Bwana, muombe Bwana, onana na watu wazima wewe
kijana, omba ushauri, usikate tamaa," amesema
Mchungaji Mang'wenhula
Akiendelea na mahubiri yake, ameeleza kuwa moja ya
changamoto kubwa inayokabili jamii na serikali ni kuongezeka kwa visa vya
kuvunjika kwa ndoa, jambo ambalo limekuwa likiathiri saikolojia ya wazazi na
jamii kwa ujumla huku akiwataka waumini kuwa na subira na kuepuka kuvunja ndoa
bila sababu za msingi.
"Serikali yetu inalalamika watu wanavunja
ndoa ovyo kwa sababu watu hawakai meza moja na kusameheana niombe vijana wa
kanisani masuala ya kuvunja ndoa yawe ni marufuku, kwa sababu mnaharibu
saikolojia ya wazazi na mnaharibu saikolojia ya serikali," .
Mchungaji Mang'wenhula amewashauri vijana ambao
wanakabiliwa na migogoro katika ndoa zao kutafuta ushauri kutoka kwa viongozi
wa kiroho na watu wazima wenye hekima badala ya kuamua kuvunja ndoa. "Kama kuna mgogoro, kwa nini msikae
meza moja? Kwa nini msitafute watu wa kuwashauri? Maana tunaowashauri nasaha
wengi katika jamii na katika kanisa," amesema.
Wakati huo huo amewatia moyo waumini kwamba ingawa majaribu ni sehemu
ya maisha ya kila mmoja, kumkabidhi Yesu Kristo ndiyo njia pekee ya kushinda
changamoto hizo.
"Mungu
atusaidie sana, majaribu tunaweza tukapata lakini tumkabidhi Yesu Kristo
atatushindia na atatutengenezea mlango wa kutokea,"
amesema.
Mchungaji
Charles Lugembe wa Kanisa la AICT Kambarage akiwahimiza waumini wa kanisa hilo
kujitokeza kwa wingi kwenye zoezi la kujiandikisha wapiga kura.
Mchungaji mstaafu wa Kanisa la AICT Ndala, Zabron
Mang'wenhula akihubiri kwenye ibada ya leo Jumapili Agosti 18,2024 katika
Kanisa la AICT Kambarage.
Mchungaji mstaafu wa Kanisa la AICT Ndala, Zabron
Mang'wenhula akihubiri kwenye ibada ya leo Jumapili Agosti 18,2024 katika
Kanisa la AICT Kambarage.
Post a Comment