
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga, Dkt. Moshi Lyoba, akielezea hali za majeruhi.
Na Mapuli Kitina Misalaba
Watu 21 walipata majeraha katika ajali ya barabarani
iliyohusisha mabasi mawili, LBS na Happy Nation, jana majira ya saa kumi jioni
katika eneo la Ibadakuli, Manispaa ya Shinyanga kati yao mwanamke mmoja aitwaye
Christina Masanja mwenye umri wa miaka 37 mkazi wa Tabora, alifariki dunia
wakati akiendelea kupatiwa matibabu.
Akizungumza na Misalaba Media, Mganga Mfawidhi wa
Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga, Dkt. Moshi Lyoba, amesema katika Hospitali
hiyo walipokea majeruhi 21, wakiwemo
wanawake nane (8), wanaume kumi na watatu (13), na watoto wawili.
Dkt. Lyoba ameeleza kuwa majeruhi wengi walikuwa na
mifupa iliyovunjika na vidonda sehemu mbalimbali za miili yao.
"Tuliwapatia
matibabu ya haraka majeruhi hao, lakini kwa bahati mbaya, mmoja wao, mwanamke
aitwaye Christina Masanja mwenye umri wa miaka 37 na mkazi wa Tabora, alifariki
dunia wakati tukiendelea kumpatia matibabu kutokana na majeraha makubwa
aliyopata kichwani," amesema Dkt. Lyoba.
Aidha, Dkt. Lyoba amebainisha kuwa wagonjwa wanne
walihamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Mwawaza, kutokana na
hali zao kuwa mbaya zaidi.
Miongoni mwao ni mgonjwa aliyevunjika mfupa, mwingine
aliyevunjika nyonga, na mtoto mwenye umri wa miaka mitano ambaye amevunjika
mkono, ambao wanahitaji matibabu maalum.
"Wagonjwa
waliobaki wamelazwa wodini na hali zao zinaendelea kuimarika, lakini
tunatarajia kuwapa rufaa wagonjwa watatu kwenda Hospitali ya Rufaa kwa matibabu
zaidi," amesema Dkt. Moshi
Wananchi walioshuhudia ajali hiyo wamewasihi madereva kuwa makini barabarani na kuzingatia sheria za usalama ili kuepusha ajali huku wakiliomba jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani kutekeleza wajibu wao ipasavyo ili kuzuia ajali.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga,
Dkt. Moshi Lyoba, akizungumza na Misalaba Media.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga, Dkt. Moshi Lyoba, akizungumza na Misalaba Media.
TAZAMA HAPA PICHA ZA MABASI MAWILI YALIYOPATA AJALI MKOANI SHINYANGA
Post a Comment