Na Mapuli Kitina Misalaba
Mashindano ya mpira wa miguu ya Krismas Cup,
yaliyoandaliwa na Makamba Mussa Lameck, yameendelea leo katika uwanja wa Mhangu
kwa nusu fainali ya kwanza kati ya Beya FC na Kano FC.
Mchezo huo umemalizika kwa ushindi wa Beya FC
kupitia mikwaju ya penalti, baada ya dakika 90 za mchezo kumalizika bila kufungana.
Kwa matokeo hayo, Beya FC imekata tiketi ya kucheza
fainali ya mashindano hayo. Akizungumza baada ya mechi hiyo, msimamizi wa ligi
hiyo, Mwalimu Emmanuel Enock Kijida, amesema nusu fainali ya pili itapigwa
kesho, ikizikutanisha Salawe FC na Mwasenge FC, na mshindi atakutana na Beya FC
kwenye fainali.
“Kwa
matokeo haya, Beya FC wamefuzu kuingia fainali na wanaenda kukutana na mshindi
wa mechi ya kesho. Timu zilizopoteza leo na zitakazopoteza kesho zitacheza
Jumatatu kumtafuta mshindi wa tatu,” amesema Mwalimu
Kijida.
Aidha, ametoa wito kwa wachezaji kuhakikisha
wanacheza kwa amani, nidhamu, na kuheshimu waamuzi, akisisitiza kuwa mashindano
haya yanalenga kukuza vipaji na kuimarisha maendeleo ya michezo katika mkoa wa
Shinyanga.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa Sungusungu, mzee Moto
Mussa Kalamji, amepongeza mwandaaji wa ligi hiyo, Makamba Mussa Lameck, kwa
juhudi zake za kudumisha utamaduni wa michezo.
“Kwanza
nimshukuru kijana wetu mpendwa Makamba kwa kazi kubwa aliyoifanya. Hii ni
burudani muhimu kwa wananchi wetu na inakuza michezo. Ninazipongeza timu zote,
hasa Beya FC, lakini niwaonye kwamba kazi bado haijaisha. Wakae mguu sawa
kuelekea fainali,” amesema mzee Moto.
Fainali za Krismas Cup zinatarajiwa
kufanyika Jumanne, Desemba 17, 2024, ambapo zawadi mbalimbali zitatolewa kwa
washindi wa nafasi ya kwanza hadi ya tatu.
Mashindano haya yanadhaminiwa na kampuni ya MCL,
inayomilikiwa na Makamba Mussa Lameck, ambayo inajihusisha na biashara ya
nafaka, ikiwa ni juhudi za kuchochea maendeleo ya michezo mkoani Shinyanga.
Post a Comment