KATIKA kuunga mkono jitihada za Serikali kwenye kuboresha sekta ya Elimu, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama Pori (TAWA) pamoja na Kampuni ya Bushman Safari wamekabidhi Madawati 160 katika Halmashauri ya Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu.
Thamani hizo zimetolewa kwa ajili ya Shule ya Sekondari ya Lung'wa na Shule za Msingi Tatu zilizopo katika Kata ya Mwaswale ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji kwa Wanafunzi.
Aidha, Mamlaka ya Uhifadhi wa Wanyamapori na Kampuni ya Bushman wamekuwa wadau muhimu Kwa Wanaitilima, hususani kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa Hifadhi ya pori la hakiba la Maswa.
Akikabidhi Madawati hayo Mwakilishi Kutoka TAWA, Mhifadhi Lusato Masinde alisema wamekuwa na destuti ya kuboresha miundombinu kwenye maeneo yanayopakana na pori la Akiba la Maswa.
"TAWA na Bushman kama wadau wa Uhifadhi wamekua na desturi ya kuhakikisha wananchi wanaoishi kandokando mwa hifadhi wana nufaika na hifadhi kwa kuboreshewa huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo Elimu, Afya na Miundombinu ya barabara" Alisema.
Mhifadhi Masinde aliuomba uongozi wa Wilaya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi waishio kandokando mwa hifadhi ili kuepukana na ujangili, ikiwemo kuendesha shughuli za ufugaji katika hifadhi.
Akipokea madawati hayo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Itilima Mwanana Msumi aliwataka wananchi wa Lung'wa na wale wote wanaoishi kandokando mwa Hifadhi kuwa sehemu ya Uhifadhi ili kuendelea kunufaika na faida zinazotokana na uhifadhi kama kuboreshewa miundombinu ya Afya, Elimu na Barabara.
Post a Comment