" WIKI YA SHERIA YAANZA RASMI MKOANI SHINYANGA WANANCHI WATAKIWA KUJITOKEZA KUPATA HUDUMA BURE

WIKI YA SHERIA YAANZA RASMI MKOANI SHINYANGA WANANCHI WATAKIWA KUJITOKEZA KUPATA HUDUMA BURE

Na Mapuli Kitina Misalaba

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha, leo Januari 25, 2025, amezindua rasmi maadhimisho ya Wiki ya Sheria, ambayo kilele chake kitakuwa Februari 03, 2025.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga Frank Habibu Mahimbali, amesema maadhimisho hayo yana lengo la kuwaelimisha wananchi kuhusu namna Mahakama inavyofanyakazi chini ya nguzo tatu za mpango mkakati wa Mahakama.

“Wataalam wetu, wakiwemo mahakimu, majaji, wasajili, na maafisa wengine wa Mahakama, wataeleza taratibu za kufungua mashauri Mahakamani, namna ya utoaji ushahidi, ukazaji wa hukumu, na maamuzi yanayotolewa pia wananchi watapata nafasi ya kutoa maoni na malalamiko yao,” amesema Jaji Mahimbali.

Amebainisha kuwa huduma zote zinazotolewa kwenye mabanda mbalimbali ni bure na amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi ili kufaidika na fursa hiyo ambapo elimu itatolewa katika maeneo mengine ikiwemo shuleni, sokoni, kwenye biashara mbalimbali, vituo vya bodaboda, na maeneo mengine ya kijamii.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni: “Tanzania 2050: Nafasi ya Taasisi Zinazosimamia Haki Madai katika Kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo.”

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha, amepongeza juhudi za Mahakama katika kuwahudumia wananchi huku akiahidi ushirikiano wa serikali.
“Sisi, kama mhimili wa utawala, tutaendelea kushirikiana nanyi kwa ukaribu ili kuhakikisha haki inatamalaki haki ikitamalaki, tutakuwa na taifa lenye amani, maendeleo, na ustawi wa wananchi,” amesema RC Macha.

Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, akitoa salamu zake, amepongeza hatua za Mahakama katika kuleta mapinduzi na maboresho ya huduma.
“Tunaendelea kuwakaribisha wananchi kujionea huduma mbalimbali za kimahakama Wilaya yetu ni mahali salama, hivyo nawahakikishia usalama wao watakapokuja kushiriki maadhimisho haya,” amesema DC Mtatiro.

Baadhi ya wananchi waliopata huduma hizo wameeleza kuridhishwa na huduma za haraka na bure zinazotolewa, huku wakitoa wito kwa wengine kujitokeza ili kupata suluhisho la changamoto zao.

Maadhimisho ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria nchini hufanyika kila mwaka, yakilenga kuashiria mwanzo wa shughuli za Mahakama baada ya likizo ya Mahakama inayomalizika Januari 31.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha, akizungumza wakati akizindua maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini kwa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga leo Januari 25, 2025.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha, akizungumza wakati akizindua maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini kwa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga leo Januari 25, 2025.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Frank Mahimbali akizungumza kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini kwa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga leo Januari 25, 2025.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Frank Mahimbali akizungumza kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini kwa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga leo Januari 25, 2025.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro akizungumza wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini kwa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga.Viongozi mbalimbali.




 

Post a Comment

Previous Post Next Post