Na, Egidia Vedasto, Misalaba Media, Arusha.
Kiwango cha Magonjwa yasiyoambukiza kimetajwa kuwa juu katika hospitali ya Rufaa ya Mount Meru iliyopo Jijini Arusha, huku sababu ikitajwa kuwa na mfumo wa maisha.
Akizungumza na Waandishi wa habari hospitalini hapo katika Kikao cha robo mwaka Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Alex Elnest ameitaka jamii kubadilisha mtindo wa maisha kwa kula vyakula vyenye mlo kamili vinavyojenga mwili ili kuepuka magonjwa hayo yanayotumia gharama kubwa na kupunguza nguvu kazi ya taifa.
"Inatupasa kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuhakikisha tunamaliza tatizo hili, unaweza kuona kwa miezi mitatu tumepokea Wagonjwa wa Kisukari 1485 na Shinikizo la damu 1173, kwa takwimu hizi inatosha kila mmoja kuona ni namna gani tatizo linazidi kuwa kubwa" amefafanua Dkt. Alex.
Aidha ameeleza kuwa wagonjwa wa kulazwa wanaoongoza hospitalini hapo wametokana na ajali za barabarani zilizosababishwa na pikipiki na magari jumla zikiwa 249 kati ya hizo ajali 198 ni mivunjiko mbalimbali
Katika hatua nyingine amesema wapo katika maboresho makubwa ya huduma za afya ikiwemo ununuzi wa vifaa tiba pamoja na ujenzi wa majengo ya kutolea huduma.
"Mwezi wa tano mwaka huu jengo la kutoa dawa za Kansa litaanza kufanya kazi ambalo litakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa 20 kwa siku, kwa sasa wananchi wanalazimika kwenda mbali kama KCMC na Ocean Road",
"Sambamba na hilo ujenzi wa jengo la upasuaji kwa njia ya matundu unaendelea na huduma hii itaanza mwezi wa kumi mwaka huu, na ujenzi wa jengo la damu salama litakamilika ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa, kwani kwa sasa sampuli za damu hupelekwa hospitali ya Kanda ya KCMC kwa ajili ya uchakataji" amefafanua Dkt Alex.
Post a Comment