Karagwe, Kagera
Mradi mkubwa wa maji wa Rwakajunju unaotekelezwa wilayani Karagwe, mkoani Kagera, umefikia asilimia 70 ya utekelezaji wake, licha ya kuwepo kwa changamoto zinazoibua maswali mazito kuhusu kasi na ubora wa kazi zinazofanywa na mkandarasi.
Mradi huo ulianza kutekelezwa April, 2023 kama sehemu ya mpango wa Serikali wa kuboresha huduma ya maji katika miji 28 nchini, na kwa mujibu wa mkataba ulipaswa kukamilika Desemba 2025. Unatekelezwa na mkandarasi Afcons JV Vijeta Infrastructure Ltd kutoka nchini India kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 64.
Mradi unatarajiwa kunufaisha wakazi wapatao 352,790 kutoka vijiji 34 vilivyopo katika kata 12 za wilaya ya Karagwe, maeneo ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakikabiliwa na uhaba mkubwa wa maji safi na salama.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi Januari 16, 2026, kwa Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, Mhandisi Magreth Nyange ambaye ni msimamizi wa mradi kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA), alisema kuwa baadhi ya kazi zimepiga hatua nzuri huku nyingine zikisuasua.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ujenzi wa chanzo cha kuzalisha maji chenye uwezo wa lita milioni 17 kwa siku umefikia asilimia 32, Ujenzi wa laini kuu ya bomba lenye kipenyo cha milimita 400 kutoka kwenye chanzo cha maji hadi eneo la kutibu maji, lenye urefu wa kilomita 1.8, umefikia asilimia 87.
Aidha, ujenzi wa tenki la maji lenye ujazo wa lita milioni 5 umekamilika kwa asilimia 83, huku uchimbaji na ulazaji wa bomba kuu lenye urefu wa kilomita 33 ukifikia asilimia 85. Hata hivyo, ujenzi wa mitambo ya kutibu maji yenye uwezo wa kuchakata lita milioni 16.5 kwa siku umefikia asilimia 45 pekee.
Hali hiyo, ilimfanya Naibu Waziri wa Maji kuhoji sababu za kusuasua kwa ujenzi wa eneo la kutibu maji pamoja na intaki ya kuchotea maji, ambayo imefikia asilimia 30, maswali ambayo hayakupatiwa majibu ya kuridhisha.
Pia alihoji kuhusu ununuzi wa mitambo ya kusukuma maji na mitambo ya umeme inayopaswa kusimikwa kwenye chanzo cha maji na eneo la kutibu maji. Mkandarasi mshauri alieleza kuwa mitambo hiyo tayari imetengenezwa na kusafirishwa na kwa sasa ipo katika bandari ya Dar es Salaam.
Hata hivyo, mkandarasi alishindwa kuwasilisha nyaraka za kuthibitisha kuwa mitambo hiyo imewasili nchini. Zaidi ya hapo, Naibu Waziri alihoji kwa nini mitambo ilinunuliwa bila kuwashirikisha wataalamu kutoka Wizara ya Maji au BUWASA kwenda kukagua kama inakidhi vigezo vya mkataba wakati wa utengenezaji nchini India, suala ambalo nalo halikupatiwa majibu.
Akizungumza katika eneo la mradi, Mhandisi Kundo Mathew alisema kuwa atafika binafsi katika bandari ya Dar es Salaam kujiridhisha kuhusu uwepo wa mitambo hiyo. Aliongeza kuwa baada ya kuthibitisha, Serikali itafanya ukaguzi wa kina ili kuhakikisha mitambo hiyo inakidhi masharti ya mkataba kabla ya kufungwa na kutumika.
Naibu Waziri pia aliibua wasiwasi juu ya nyongeza ya muda wa miezi tisa aliyopewa mkandarasi kukamilisha mradi huo, akisema ni vigumu kuelewa kama ataweza kukamilisha kazi hiyo ilhali awali alipewa muda wa miaka miwili lakini ameshindwa kumaliza kwa wakati.
Naibu Waziri maji aliulizwa na waandishi kuwa sintofahamu na maswali ambayo hayakujibiwa na mkandarasi inatosha kuwaeleza wananchi kuwa mradi huo umekwama?Naibu Waziri alijibu mradi haujakwama ila alieleza kuna uzembe ambao unafanyika na hakueleza wazi uzembe huo unafanywa na nani.
Kwa upande wao, wananchi wameendelea kuonesha masikitiko yao. Wakizungumza na mwandishi wetu, Evarister Clemens Murashani na Joas Maliseri, wakazi wa Kijiji cha Nyakashenyi, kata ya Nyabiyonza wilayani Karagwe, walisema walikuwa na matumaini makubwa kwamba mradi huo ungeanza kutoa maji mwishoni mwa mwaka 2025 kama walivyoahidiwa.
“Tuliahidiwa maji safi na salama, lakini hadi sasa bado tunaendelea kutaabika. Tunaona miradi iko katikati, lakini maji hayatoki,” alisema Murashani.
Wananchi hao wameiomba Serikali kusimamia kwa karibu mradi huo ili ukamilike haraka na kuondoa adha ya muda mrefu ya ukosefu wa maji safi na salama katika maeneo yao
Mwisho.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254




Post a Comment