Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Palamagamba Kabudi akitoa hotuba wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji Tanzania ' Annual Broadcaster's Conference'
Na Mapuli Kitina Misalaba
Serikali imesema itaendelea kushirikiana na vyombo
vya habari nchini ili kuhakikisha vinafanya kazi kwa uhuru na weledi kuelekea
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Kauli hiyo imetolewa leo Februari 13, 2025, na
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi, wakati
akifungua Mkutano wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji Tanzania Annual
Broadcasters’ Conference, unaofanyika jijini Dodoma kwa siku mbili.
"Niwaahidi kuwa wizara
ninayoiongoza itawapa ushirikiano wote mnaouhitaji ili kuleta matokeo chanya
katika sekta ya habari, utamaduni, sanaa na michezo,"
amesema Prof. Kabudi.
Waziri Kabudi amesema Serikali inayoongozwa na Dkt.
Samia Suluhu Hassan inaendelea kushughulikia changamoto mbalimbali
zinazoikabili sekta ya habari na kuahidi kuwa wizara yake itatoa ushirikiano
unaohitajika ili kuhakikisha vyombo vya habari vinatoa mchango chanya kwa
taifa.
Prof. Kabudi pia amesisitiza umuhimu wa vyombo vya
habari kutoa maudhui yenye tija kwa jamii badala ya kuangazia burudani pekee,
huku akiwakumbusha waandishi kuzingatia weledi na kuacha kusambaza habari za
upotoshaji.
Katika mkutano huo ulioandaliwa na Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA), wadau wa sekta ya habari wamejadili wajibu wa
vyombo vya utangazaji katika kulinda haki, usawa, na weledi wa habari kuelekea
uchaguzi mkuu.
Prof. Kabudi pia amewataka watangazaji kutumia
Kiswahili fasaha na sanifu badala ya kuvuruga maneno na kuharibu ufasaha wa
lugha.
"Vyombo vya habari vina jukumu
kubwa la kuelimisha umma, lakini tumeshuhudia mabadiliko ya matumizi ya
Kiswahili yasiyo sahihi. Ni jukumu lenu kurudisha heshima ya lugha yetu,”
amesema Kabudi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabir
Bakari, amesema mkutano huo unatoa nafasi kwa wadau wa utangazaji kujadili
changamoto za sekta hiyo na kubuni mbinu za kuboresha huduma za utangazaji
nchini.
Naye Msemaji Mkuu wa Serikali, Grayson Msigwa,
amewakumbusha waandishi wa habari kuwa na umakini mkubwa katika matumizi ya
teknolojia za kisasa, hususan Akili Bandia (AI), ili kuhakikisha taarifa
zinazochapishwa au kutangazwa haziwezi kupotosha umma.
Mkutano huo utaendelea hadi Februari 14, 2025,
ambapo mada mbalimbali kuhusu mustakabali wa sekta ya utangazaji kuelekea
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 zitajadiliwa.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabiri Bakari, akizungumza
kwenye mkutano wa Mwaka wa vyombo vya utangazaji, leo Februari 13, 2025.























Post a Comment