Katibu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mpanda, Jimotoli Jilala Maduka, akiwa pamoja na Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya hiyo, wametembelea Shule ya Sekondari ya Milala, inayomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda, kwa lengo la kukagua miundombinu na kujionea hali ya mazingira ya shule hiyo.
Katika ziara hiyo, Katibu na wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji walipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya shule, ikiwa ni pamoja na madarasa, mabweni, ofisi na maeneo ya wazi, ili kubaini hali halisi ya miundombinu na mahitaji muhimu yanayohitaji maboresho kwa ajili ya maendeleo ya shule.
Baada ya ukaguzi huo, Kamati imebaini changamoto kadhaa zinazohitaji hatua za haraka ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia katika shule hiyo, ikiwa ni pamoja na ukarabati wa baadhi ya majengo na upatikanaji wa vifaa muhimu vya elimu.
Kutokana na hali hiyo, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda, Jimotoli Jilala Maduka, amewaomba wawekezaji kujitokeza ili kuwekeza katika shule hiyo, kwa lengo la kuimarisha miundombinu na kuinua kiwango cha elimu.
"Tunawakaribisha wawekezaji wenye mapenzi mema kushirikiana nasi katika kuendeleza shule hii ya Milala ili kuhakikisha tunatoa elimu bora kwa watoto wetu. Huu ni wakati wa kuonesha uzalendo kwa vitendo," amesema Katibu Jilala Maduka.
Post a Comment