" CCM YAZINDUA RASMI ILANI YA UCHAGUZI MKUU 2025

CCM YAZINDUA RASMI ILANI YA UCHAGUZI MKUU 2025

 

CCM Yazindua Rasmi Ilani ya Uchaguzi Mkuu 2025

Na Marco Maduhu.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimezindua rasmi Ilani yake ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, katika Mkutano Mkuu Maalum uliofanyika leo mei 30,2025 kwenye Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma.

Uzinduzi huo umeongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ilani ya CCM, Profesa Kitila Mkumbo, alisema Ilani hiyo ya uchaguzi kwa kipindi cha 2025 hadi 2030 imeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya wananchi na dira ya maendeleo ya taifa.

Amesema Ilani hiyo imebeba vipaumbele tisa, ikiwamo kuboresha maisha ya watu, kuimarisha ustawi wa jamii, na kuendelea kupunguza umaskini nchini.

“Vipaumbele vingine ni kuchochea mapinduzi ya kisiasa yaliyo jumuishi, shindani na fungamanishi, kuongeza thamani ya rasilimali za ndani, pamoja na kupanua fursa za ajira kwa vijana na kuongeza kipato cha wananchi,” amesema Prof. Mkumbo.

Ilani hiyo inatarajiwa kuwa nyenzo kuu ya kampeni za chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ambapo CCM inalenga kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika awamu zilizopita.

Post a Comment

Previous Post Next Post