Na Mapuli Kitina Misalaba
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius
Mtatiro, amevionya vikali vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu
walionufaika na mikopo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, akisisitiza
kuwa serikali haitasita kuchukua hatua kali, ikiwemo kifungo cha jela, kwa wale
watakaoamua kugeuza matumizi ya fedha hizo kinyume na makubaliano ya awali.
Akizungumza leo Mei 27, 2025, wakati
wa hafla ya uzinduzi wa utoaji wa mikopo ya awamu ya pili kwa vikundi
vilivyokidhi vigezo, Mtatiro amesema serikali imejitoa kwa dhati kuwainua
wananchi kiuchumi kupitia mikopo hiyo isiyo na riba, hivyo ni wajibu wa
wanavikundi kuhakikisha fedha hizo zinatumika kama ilivyokusudiwa.
“Tunapotoa fedha hizi, tunatarajia
zielekezwe katika malengo yaliyowasilishwa kwenye maombi ya mkopo. Kama kuna
mtu ndani ya kikundi atataka kutumia fedha kwa shughuli binafsi au tofauti na
walivyokubaliana, serikali itamchukulia hatua kali ikiwemo kumfikisha
mahakamani na kumfungia jela,”
amesema Mtatiro kwa msisitizo.
Aidha, amewataka wanavikundi
kushirikiana kwa karibu katika utekelezaji wa miradi yao na hasa katika
matumizi ya fedha, huku akitoa pongezi kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya
ya Shinyanga, Dkt. Kalekwa, watumishi wa halmashauri hiyo, Mwenyekiti wa
Halmashauri na baraza la madiwani kwa kusimamia vyema mapato ya ndani hali
iliyosababisha halmashauri hiyo kuvuka malengo ya makusanyo kwa zaidi ya
asilimia 100.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Dkt. Kalekwa Kasanga, amevitaka vikundi
hivyo kuwa na juhudi katika biashara na miradi yao ili kuhakikisha wanaongeza
tija na kupata faida, huku akisisitiza umuhimu wa nidhamu ya kifedha.
“Mkumbuke fedha hizi si za msaada,
ni mkopo. Mnapaswa kuzirudisha kwa wakati ili kuwezesha wengine kupata fursa
hii. Kama kuna mtu atataka kuingilia au kutumia fedha zenu kinyume na utaratibu,
taarifa zitolewe kwa viongozi ili hatua zichukuliwe,” amesema Dkt. Kalekwa.
Naye Mbunge wa Jimbo la Solwa, Mhe.
Ahmed Ally, amepongeza jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za maendeleo, akisema kuwa
hatua hiyo imeleta mwanga mpya wa maendeleo kwa wananchi wa jimbo lake.
Mbunge huyo amevihimiza vikundi
kurejesha mikopo kwa wakati ili kuendelea kunufaika katika awamu zijazo, huku
akiwasihi wananchi kuendelea kumwamini na kumuunga mkono Rais Samia katika kila
hatua.
“Nawaomba wananchi tuendelee
kumuunga mkono Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kumpigia kura nyingi ifikapo
wakati wa uchaguzi, ili aendelee na kazi nzuri ya kuwaletea maendeleo. Pia ni
muhimu jimbo hili liendelee kuwa na mbunge wa CCM ili tushirikiane vizuri
katika kusukuma gurudumu la maendeleo,”
amesema Ahmed.
Akiwasilisha taarifa ya mikopo hiyo,
Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga,
Joseph Ntomela amesema mikopo hiyo inatolewa kwa mujibu wa agizo la serikali na
kufuatia maboresho ya taratibu za usimamizi wa mikopo isiyo na riba kwa
wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Katika awamu ya kwanza, Halmashauri
ya Wilaya ya Shinyanga ilitoa mikopo yenye jumla ya Tsh 152,500,000 kwa vikundi
15 vilivyokidhi vigezo: ambapo Vikundi vya wanawake: 8 – Tsh 81,500,000 huku Vikundi
vya vijana: 7 – Tsh 71,000,000
Katika awamu ya pili (Januari –
Machi 2025), vikundi 94 vilisajiliwa, vikiwa na jumla ya maombi ya mkopo
yenye thamani ya Tsh 2,452,468,300. Baada ya uhakiki, vikundi 56 pekee ndivyo
vilivyokidhi vigezo na kupatiwa mikopo yenye jumla ya Tsh 537,800,000:
Vikundi vya wanawake: 32 – Tsh
310,100,000, Vikundi vya vijana: 20 – Tsh 209,400,000 na Vikundi vya watu wenye
ulemavu: 4 – Tsh 18,300,000
Baada ya kupokea hundi zao,
wanavikundi wanapewa mafunzo maalum yatakayowasaidia katika utekelezaji wa
miradi yao. Mafunzo haya yanajumuisha mada zifuatazo:
Utunzaji wa kumbukumbu na uwekaji wa akiba, Usimamizi
wa miradi ya kilimo na mifugo, Ujasiriamali na masoko, Uendeshaji wa vikundi, Uzalendo
katika usimamizi wa mali, Taratibu za kurejesha mkopo, Mipango ya maendeleo, Sheria
na kanuni za mikopo, Wajibu na haki za wanakikundi na Utatuzi wa migogoro ya
kikundi
Miongoni mwa vigezo vya msingi ili
kikundi kuwa na safia ya kupata mkopo ni: Wanakikundi wawe raia wa Tanzania, Umri
wa vijana kati ya miaka 18 hadi 45,
Kikundi
kiwe kimesajiliwa katika mfumo wa serikali,
Kikundi
kiwe na akaunti ya benki, Kisiwe na wanachama wenye ajira
rasmi ambapo kwa watu wenye
ulemavu, kuwe na walau wanakikundi wawili







Mbunge wa Jimbo la Solwa, Mhe. Ahmed
Ally, akizungumza leo Mei 27, 2025, wakati wa hafla ya uzinduzi wa utoaji wa
mikopo ya awamu ya pili kwa vikundi vilivyokidhi vigezo katika Halmashauri ya
Wilaya ya Shinyanga.











Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya
ya Shinyanga Mhe. Ngassa Mboje akizungumza leo Mei 27, 2025, wakati wa hafla ya
uzinduzi wa utoaji wa mikopo ya awamu ya pili kwa vikundi vilivyokidhi vigezo
katika Halmashauri hiyo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya
ya Shinyanga Mhe. Ngassa Mboje akizungumza leo Mei 27, 2025, wakati wa hafla ya
uzinduzi wa utoaji wa mikopo ya awamu ya pili kwa vikundi vilivyokidhi vigezo
katika Halmashauri hiyo.

Post a Comment