Na Mapuli Kitina Misalaba
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha
ameongoza maelfu ya wafanyakazi kutoka taasisi mbalimbali katika maandamano ya
amani ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani
yanayofanyika leo Mei 1, 2025.
Maandamano hayo yameanzia katika viwanja vya
Zimamoto mjini Shinyanga na kuelekea uwanja wa CCM Kambarage ambako sherehe za
kimkoa zinaendelea kwa shamrashamra mbalimbali zikiwemo burudani na utoaji wa
zawadi kwa wafanyakazi bora.
Wafanyakazi kutoka Halmashauri zote sita za Mkoa wa
Shinyanga — Manispaa ya Kahama, Manispaa ya Shinyanga, Halmashauri ya Wilaya ya
Ushetu, Kishapu, Msalala pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga — wamejitokeza
kwa wingi kuonesha mshikamano wao katika kutambua mchango mkubwa wanaoutoa
katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Maadhimisho ya mwaka huu yamebebwa na kaulimbiu
isemayo “UCHAGUZI MKUU 2025 UTULETEE VIONGOZI WANAOJALI HAKI NA MASLAHI YA WAFANYAKAZI,
SOTE TUSHIRIKI”, ikiwa ni wito kwa Watanzania kushiriki kikamilifu katika
mchakato wa uchaguzi kwa maslahi ya wafanyakazi.



Post a Comment