" RAIS DKT SAMIA KUHUDHURIA IBADA YA KUMUAGA HAYATI CLEOPA MSUYA KILIMANJARO

RAIS DKT SAMIA KUHUDHURIA IBADA YA KUMUAGA HAYATI CLEOPA MSUYA KILIMANJARO



Na Ashrack Miraji

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kushiriki katika ibada ya kumuaga aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu, Hayati Cleopa David Msuya, leo Mei 13, 2025.

Ibada hiyo inafanyika katika Kanisa la KKKT Kristo Mchungaji Mwema; Dayosisi ya Mwanga, Jimbo la Kaskazini, Usharika wa Usangi Kivindu, Usangi, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro.

Ibada hiyo ya kumuaga mzee Msuya inatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa, wakiwemo Marais wastaafu, Mawaziri wakuu wa zamani, viongozi wa vyama vya siasa, mabalozi, na wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini. Hii ni ishara ya heshima kubwa anayopatiwa kutokana na mchango wake mkubwa kwa taifa la Tanzania katika kipindi chote cha uongozi wake.

Hayati Cleopa David Msuya atakumbukwa kama kiongozi mzalendo, mchapakazi na mwenye busara aliyeweka mbele maslahi ya taifa. Alitumikia nafasi mbalimbali za juu serikalini kwa uaminifu na hekima, ikiwemo kuwa Waziri Mkuu mara mbili na Makamu wa Kwanza wa Rais. Maamuzi yake mengi yalilenga ustawi wa Watanzania na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro, hususan wa Wilaya ya Mwanga, wameendelea kujitokeza kwa wingi kushiriki shughuli za kumuaga shujaa wao. Mazingira ya ibada yameandaliwa kwa utulivu na heshima kubwa, yakionesha mshikamano wa kitaifa katika kumuenzi mmoja wa viongozi waliotoa mchango wa kipekee kwa historia ya Tanzania.



Viongozi mbalimbali na Wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro na mikoa ya jirani, pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwasili katika Kanisa la KKKT Kristo Mchungaji Mwema; Dayosisi ya Mwanga, Jimbo la Kaskazini, Usharika wa Usangi Kivindu, mkoani Kilimanjaro, leo Mei 13, 2025, kushiriki ibada maalumu ya mazishi ya aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu, Hayati Cleopa David Msuya.

Post a Comment

Previous Post Next Post