" SHIRIKA LA HELPAGE TANZANIA LAENDESHA MAJADILIANO YA MAKUNDI RIKA WILAYANI KISHAPU KWA LENGO LA KUKOMESHA UKATILI WA KIJINSIA NA MILA POTOFU

SHIRIKA LA HELPAGE TANZANIA LAENDESHA MAJADILIANO YA MAKUNDI RIKA WILAYANI KISHAPU KWA LENGO LA KUKOMESHA UKATILI WA KIJINSIA NA MILA POTOFU


Na Mapuli Kitina Misalaba

Shirika lisilo la kiserikali la HelpAge Tanzania limeendesha mjadala wa makundi rika katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, likiwa na lengo la kukuza usawa wa kijinsia, kutokomeza mila kandamizi, na kuimarisha afya ya uzazi hasa kwa wanawake, wasichana na watu wenye ulemavu.

Tukio hilo limefanyika ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Chaguo Langu, Haki Yangu, unaofadhiliwa na Serikali ya Finland na kuratibiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) kwa kushirikiana na wizara na taasisi mbalimbali.

Akizungumza wakati wa majadiliano hayo, Leonard Ndamgoba, Mkuu wa Programu wa HelpAge Tanzania, amesema shirika hilo limeandaa mwongozo maalum wa majadiliano kati ya makundi ya wazee na vijana ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kuikumba jamii.

"Tunashukuru Serikali ya Finland kwa kufadhili mradi huu na UNFPA kwa usimamizi wa karibu. Mwongozo huu unalenga kuvunja mila potofu kama ukeketaji, ndoa za utotoni na ukatili wa kijinsia. Kupitia mijadala ya makundi rika, tunatengeneza jukwaa la kuleta mabadiliko ya kweli kutoka kizazi kimoja kwenda kingine," amesema Ndamgoba.

Ameongeza kuwa wawezeshaji waliopatiwa mafunzo wataendesha mijadala hiyo katika maeneo mbalimbali ikiwemo mikutano ya hadhara, vikundi vya vijana na wazee, na hata kwenye matukio ya kijamii kama misiba na harusi na kwamba wawezeshaji waliobobea watawajengea uwezo wawezeshaji wapya ili kuendeleza juhudi hizo kwa muda mrefu.

Majadiliano ya makundi rika pia yanajikita katika kuziba pengo kati ya vizazi tofauti kwa kuvunja mitazamo potofu ya kijinsia na kukabiliana na ukosefu wa usawa uliojengeka kwa muda mrefu. Kwa kujenga mazingira salama ya mazungumzo, wanawake na wasichana – hasa wenye ulemavu – wanapewa nafasi ya kudai haki zao katika nyanja za elimu, uchumi, afya ya uzazi na ushiriki wa kijamii.

Mratibu wa Mradi wa Chaguo Langu, Haki Yangu ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Ibrahim Sakulia, amewaomba wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha wakati wa hatua za utambuzi na utatuzi wa changamoto mbalimbali za ukatili na mila kandamizi zinazozikabili jamii.

Amesema ushirikiano wa wananchi ni msingi muhimu katika kufanikisha malengo ya mradi huo unaotekelezwa na HelpAge kwa ufadhili wa Serikali ya Finland kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA).

“Lengo letu ni kuifanya jamii ijitambue na ipate nafasi ya kujadili changamoto zinazowakabili, zikiwemo ndoa za utotoni, ukeketaji na mila kandamizi. Tunahitaji wananchi washiriki kikamilifu mijadala hii kwa sababu wao ndio chachu ya mabadiliko tunayoyakusudia,” anasema Sakulia.

Katika mafunzo hayo, wawakilishi wa makundi ya vijana na wazee kutoka kata hizo tatu wamepewa mbinu za kuendesha midahalo ya makundi rika katika maeneo yao ili kuchochea mijadala ya wazi juu ya ukatili wa kijinsia na namna ya kuukomesha kwa njia ya majadiliano, usawa wa kijinsia, na heshima kwa haki za binadamu.

Kwa upande wake, Kaimu Mratibu wa Huduma za Mama na Mtoto katika Hospitali ya Wilaya ya Kishapu, Hilda Ebunka, amesema hali ya mimba za utotoni imeonesha kupungua ukilinganisha na miaka ya nyuma, jambo linaloashiria mafanikio ya juhudi za pamoja kati ya serikali na mashirika ya kiraia.

“Tulikuwa tunapokea kesi nyingi za wasichana wadogo kupata ujauzito. Kwa sasa hali imeanza kubadilika, ingawa bado tunahitaji kuendelea na elimu kwa jamii, hasa maeneo ya vijijini,” anasema Ebunka.

Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Paul Lupolaso, amesema ofisi yake imekuwa ikipokea kesi mbalimbali za ukatili, ambapo kubwa ni pamoja na ndoa za utotoni, ukatili wa kimwili, na unyanyasaji wa kiuchumi, hasa kwa wanawake na watoto.

“Tunapokea malalamiko kutoka familia mbalimbali. Ndoa za utotoni ni changamoto kubwa kwa sababu huwakosesha watoto haki ya elimu, afya bora na maendeleo ya baadaye,” anasema Lupolaso.

Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Kishapu, Inspekta Rose Mbwambo, amesema dawati hilo limekuwa msaada mkubwa kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia, huku akitoa rai kwa jamii kushirikiana na jeshi la polisi kutoa taarifa mapema wanapobaini vitendo vya kikatili ikiwa ni pamoja na kutoa ushahidi.

“Tunahitaji jamii kushirikiana nasi kwa ukaribu. Wananchi wafahamu kuwa kazi ya dawati letu ni kusaidia siyo kuadhibu. Tunapokea taarifa, tunachunguza na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria,” anasisitiza Inspekta Mbwambo.

Ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwafundisha watoto kuhusu haki zao, na kuhakikisha wanawaweka salama dhidi ya ukatili wa aina yoyote ile.

Baadhi ya wananchi kutoka kata za Idukilo, Mwamalasa na Mwamashele wameeleza kuwa mafunzo hayo yamewapa maarifa mapya kuhusu namna bora ya kupambana na ukatili wa kijinsia na kuendesha midahalo ya makundi rika kwa lengo la kuhamasisha mabadiliko chanya kwenye jamii.

 Wananchi hao wamelishukuru shirika la HelpAge kwa kuwaleta pamoja na kuwapatia mafunzo hayo, wakiahidi kuyatumia kikamilifu katika jamii zao ili kupunguza na hatimaye kumaliza kabisa vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Shirika la HelpAge Tanzania linatarajia kuwa mwongozo huu utasaidia kuleta mabadiliko ya kijamii na kiutamaduni ambayo yatasaidia kujenga jamii yenye usawa wa kijinsia, heshima kwa haki za binadamu na uhuru kwa kila mwanajamii, wakiwemo wanawake, watoto, wazee na watu wenye ulemavu.

Mkuu wa Programu wa HelpAge Tanzania, Leonard Ndamgoba akiongoza  mjadala wa makundi rika kwa wawakilishi kutoka kata za Idukilo, Mwamalasa na Mwamashele katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.

Mkuu wa Programu wa HelpAge Tanzania, Leonard Ndamgoba akiongoza  mjadala wa makundi rika kwa wawakilishi kutoka kata za Idukilo, Mwamalasa na Mwamashele katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.


Mjadala wa makundi rika kwa wawakilishi kutoka kata za Idukilo, Mwamalasa na Mwamashele katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga ukiendelea.


Mratibu wa Mradi wa Chaguo Langu, Haki Yangu  ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Ibrahim Sakulia, akieleza hali ya ukatili wa kijinsia katika Wilaya ya Kishapu.

Mratibu wa Mradi wa Chaguo Langu, Haki Yangu  ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Ibrahim Sakulia, akieleza hali ya ukatili wa kijinsia katika Wilaya ya Kishapu.



Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Paul Lupolaso, akizungumza kwenye mjadala huo wa makundi rika ambao umeratibiwa na shirika la HelpAge Tanzania kupitia mradi wa Chaguo langu, Haki yangu.

Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Paul Lupolaso, akizungumza kwenye mjadala huo wa makundi rika ambao umeratibiwa na shirika la HelpAge Tanzania kupitia mradi wa Chaguo langu, Haki yangu.

 Kaimu Mratibu wa Huduma za Mama na Mtoto katika Hospitali ya Wilaya ya Kishapu Hilda Ebunka, akizungumza kwenye mjadala huo wa makundi rika ambao umeratibiwa na shirika la HelpAge Tanzania kupitia mradi wa Chaguo langu, Haki yangu.

Mjadala wa makundi rika ukiendelea katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu.

Edward Nangi akiwasilisha taarifa ya mradi kutoka kata ya Mwamalasa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga. 
Edward Nangi akiwasilisha taarifa ya mradi kutoka kata ya Mwamalasa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga. 
Antony Francis mkazi wa kata ya Mwamashele akizungumza kwenye mjadala huo.









 

Post a Comment

Previous Post Next Post