
John Bukuku na Meleka Kulwa, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema chama cha Mapinduzi Mei 30, 2025 kitazindua rasmi Ilani ya Uchaguzi ya (CCM) kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, 2025 hadi 2030, katika Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Taifa unaoendelea jijini Dodoma.
Akizungumza katika siku ya kwanza ya mkutano mkuu maalum wa CCM unaofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Conversation Center, Rais Samia amesema Ilani hiyo mpya imeandaliwa kwa kuzingatia changamoto, mafanikio, na matarajio ya Watanzania, ikiwa na lengo la kuharakisha maendeleo jumuishi na endelevu katika sekta zote muhimu za Taifa.
“Ilani hii si hati ya ahadi tu, bali ni mkataba wa matumaini kati ya CCM na wananchi wote wa Tanzania. Tumejipanga vizuri zaidi, kwa vitendo,” alisisitiza Rais Samia.
Ilani ya 2025–2030 inalenga kuendeleza mafanikio ya serikali ya awamu ya sita katika maeneo kama afya, elimu, miundombinu, kilimo, viwanda, nishati, maji, na huduma za kijamii. Pia imeweka msisitizo kwenye maendeleo ya sayansi na teknolojia, usawa wa kijinsia, na ustawi wa vijana na watu wenye ulemavu.
Katika hotuba yake, Rais Samia alieleza kuwa maandalizi ya Ilani hiyo yalihusisha maoni ya wananchi kutoka pande zote za Muungano, yakiongozwa na wataalamu wa sekta mbalimbali pamoja na wanachama wa CCM walioko mashinani.
Rais pia aligusia mafanikio ya chama katika kipindi cha nyuma, akitaja usajili wa wanachama wapya zaidi ya milioni 13 Tanzania Bara na Zanzibar kuwa ni kielelezo cha imani ya wananchi kwa CCM.
Aidha, alibainisha kuwa chama kimefanya maboresho ya Katiba yake ili kuongeza ufanisi, ikiwemo kuweka taratibu mpya za uteuzi wa wagombea Urais na Mgombea Mwenza kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Uzinduzi wa Ilani hii unafuatia hatua nyingine muhimu zilizochukuliwa na CCM katika siku zilizopita, ikiwa ni pamoja na uzinduzi wa ujenzi wa jengo jipya la Makao Makuu ya CCM katika mtaa wa Salmin, jijini Dodoma – mradi mkubwa wa ghorofa tano unaotarajiwa kukamilika mwaka 2027 kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 34.
Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Taifa unaendelea kwa siku mbili, ukijadili mwelekeo wa chama katika uchaguzi mkuu ujao na nafasi yake katika kuendeleza misingi ya demokrasia na maendeleo ya Taifa.









Post a Comment