Na Mapuli Kitina Misalaba
Umoja wa Wanaume Mkoa wa Shinyanga umetumia mdahalo
wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Familia kutoa wito kwa wanaume kushiriki
kikamilifu katika malezi na makuzi ya watoto ili kujenga familia bora na taifa
imara.
Akizungumza katika mdahalo huo uliofanyika kwenye
ukumbi wa mikutano wa Manispaa ya Shinyanga, Katibu wa Umoja huo, Mzee Nsolo
Stephen, amesema bado kuna changamoto kubwa ya wanaume wengi kujiondoa kwenye
majukumu ya msingi ya malezi na kuacha mzigo huo kwa wanawake pekee.
“Kuna haja kubwa ya mabadiliko ya mtazamo katika
jamii. Wanaume hawapaswi kuonekana kama wahudumu wa mahitaji ya kifedha tu,
bali washiriki wa moja kwa moja katika malezi ya watoto wao,” amesema Mzee
Nsolo.
Kwa upande wake, Katibu Msaidizi wa Umoja huo, Simeo
Makoba, amesisitiza kuwa jukumu la malezi ni la pamoja na linahitaji
ushirikiano kati ya baba na mama ili mtoto akue katika mazingira yenye upendo,
maadili na uelewa.
“Ukosefu wa ushiriki wa baba katika malezi
umesababisha mmomonyoko wa maadili kwa baadhi ya watoto. Tunapaswa kurejesha
misingi ya familia zenye mshikamano,” amesema Makoba.
Umoja huo umetoa wito kwa jamii kuondoa dhana potofu
kuwa malezi ni kazi ya wanawake pekee na badala yake kujenga utamaduni wa
kushirikiana kuanzia ngazi ya familia.



Post a Comment